Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 153 wanaodaiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya jinai, katika misako na operesheni zinazoendelea kufanyika kwa lengo la kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu mkoani humo.
Taarifa hiyo imetolewa na kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa polisi Janeth Magomi ambapo amesema mbali na watuhumiwa hao, Jeshi hilo pia limewakamata wahamiaji haramu 47 katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga, wakidaiwa kuingia na kuishi nchini bila kuwa na vibali halali.
Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi pia limekamata vielelezo mbalimbali vinavyohusishwa na makosa hayo, ikiwemo noti bandia zenye thamani ya Shilingi milioni 1.53, mirungi kilogramu 43, bangi yenye uzito wa kilogramu 380, pikipiki 26, mifuko 13 ya saruji, nondo 20, mbao 70, baiskeli moja pamoja na mtungi mmoja wa kuzimia moto.
Kwa upande wa mafanikio ya kesi zilizofikishwa mahakamani, jumla ya washitakiwa 24 wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo vya kuanzia miezi minne hadi miaka 30 kwa makosa mbalimbali, yakiwemo wizi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ubakaji, unyanyasaji pamoja na makosa mengine.
Baadhi ya washitakiwa hao wamehukumiwa kulipa faini, huku wakitakiwa kutumikia vifungo endapo watashindwa kulipa faini walizopewa.
Katika hatua nyingine, Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga kimeendesha operesheni mbalimbali na kubaini jumla ya makosa 5,291 ya ukiukaji wa Sheria za Usalama Barabarani.
Kati ya makosa hayo, 4,079 yalihusisha magari, huku makosa 1,212 yakihusu bajaji na pikipiki. Wahusika wote wamechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kulipa faini za papo kwa papo.
Aidha, katika kipindi cha miezi mitatu, madereva sita wamefungiwa leseni zao za udereva baada ya kubainika kuendesha magari kwa mwendokasi wa kilomita 116 kwa saa.
Sambamba na operesheni hizo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia mikutano 448 iliyofanyika katika vituo vya redio, shule, vituo vya waendesha pikipiki, stendi za mabasi na minadani.
Elimu hiyo imelenga kuhamasisha jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, kuimarisha ulinzi shirikishi, kuzingatia maadili ya vijana, kuwahimiza madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewashukuru wananchi kwa kuendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya uhalifu na kudumisha amani na usalama.
Aidha, Jeshi hilo limewakumbusha madereva na watumiaji wote wa barabara kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani wakati wote ili kuepusha ajali na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment