" MANISPAA YA KAHAMA YATUNUKIWA TUZO NA MWENGE WA UHURU 2026

MANISPAA YA KAHAMA YATUNUKIWA TUZO NA MWENGE WA UHURU 2026

 




Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Masudi Kibetu, amekabidhiwa tuzo kwa kuonyesha ufanisi katika shughuli ya kusajili na kutoa kazi (tender) kwa makundi maalum kupitia mfumo wa manunuzi wa umma (NEST).


Tuzo hiyo imekabidhiwa na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2026, Wazo Mwang'onda, katika viwanja vya mkesha wa mwenge, kituo cha Malori, Majengo, Kahama, August 21,2026.


Manispaa ya Kahama ilipewa lengo la Kusajili Vikundi vya Makundi Maalum 150 kupitia NEST, lakini wamevuka lengo kwa kusajili vikundi 326 sawa na asilimia 217.


Kati ya hivyo, vikundi vya Vijana ni 173, Vikundi vya Wanawake 150, vikundi vya watu wenye ulemavu viwili na kikundi cha wazee kimoja.


Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya mkurugenzi Kibetu, afisa maendeleo ya jamii kutoka Manispaa hiyo, Mbwana Karata, amesema Halmashauri imetenga kiasi Cha Shilingi 1,943,353,500 ambayo ni asilimia 30 ya manunuzi ya Serikali.


Vikundi 4, vimetunukiwa zabuni zenye thamani ya Sh 242,450,000 kati ya hivyo Vikundi vya Vijana ni viwili vilivyopata Sh 74,450,000 na Vikundi vya Wanawake ni viwili Sh 168,000,000.


Baada ya kupokea tuzo hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Kibetu amesema kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya Umoja wa Watumishi na Viongozi wa Manispaa hiyo na Wilaya kwa ujumla.


Amesema "Kutambuliwa na PPRA kupitia tuzo hii ni ishara kwamba ushirikiano uliopo katika utekelezaji wa majukumu yetu umezaa matokeo chanya. Nawapongeza watumishi na viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha zoezi hili."


Aidha hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha makundi maalum yanapata fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia mfumo wa manunuzi ya umma, pamoja na kuwawezesha vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee kunufaika na fursa zinazotokana na matumizi ya fedha za Serikali.


Mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo wa NeST katika ununuzi wa umma, kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na ushiriki wa makundi mbalimbali katika fursa za zabuni za Serikali.


Post a Comment

Previous Post Next Post