" DIRA 2050 YASISITIZA UNYWAJI WA MAZIWA, WADAU WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI.

DIRA 2050 YASISITIZA UNYWAJI WA MAZIWA, WADAU WATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI.


Na, Egidia Vedasto,Misalaba Media, Arusha.

Mkuu wa Wilaya Longido, Salum Kalli, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema Dira ya Maendeleo 2050 inachagiza uhuru wa mtu na maendeleo binafsi, ikiwemo kujenga misingi ya lishe bora kwa kila Mtanzania sambamba na kuhakikisha wananchi wanatumia maziwa ya kutosha.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maziwa yaliyofanyika katika viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha, Kalli amesema ili kufanikisha mpango huo, ni muhimu kuimarisha ushirikiano kati ya Bodi ya Maziwa, wazazi, walezi, walimu na wadau wa maendeleo katika kuhamasisha unywaji wa maziwa.

Amesema maziwa si suala la lishe pekee, bali pia ni fursa ya kiuchumi kwa wafugaji, wasindikaji, wazalishaji wa pembejeo, wafanyabiashara na wawekezaji, hivyo hatua zaidi zinahitajika katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Aidha, Kalli amewataka wafugaji kuongeza uzalishaji na kuzingatia ubora wa malisho pamoja na usafi, huku akiitaka sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika sekta ya maziwa. Amesisitiza maziwa yanywewe kwa wingi majumbani na shuleni ili kusaidia watoto kukua vizuri kiafya na kiakili na kufanya vizuri katika masomo yao.

Kwa upande wake Dr. Mackrina Nombo kutoka Wizara ya Mifugo na uvuvi amesema ni wakati wa kuachana na mfumo wa kufuga ng’ombe wengi wasio na tija na badala yake wafugaji wafuge idadi ndogo ya mifugo yenye tija kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa.

Amesema katika mradi huo kuna kitengo cha lishe kinacholenga kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya lishe na kuelewa umuhimu wa unywaji wa maziwa katika kuboresha afya na ustawi wa jamii.

"Kwa kushirikiana na Bodi ya Maziwa, tumekuwa tukitembelea shule mbalimbali kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu lishe bora na umuhimu wa kunywa maziwa, mradi huo unaendeleza mpango wa Wizara wa unywaji wa maziwa shuleni, ambapo mwaka huu jumla ya shule 18 Tanzania Bara na Visiwani zitatekeleza mpango huo".

Dr. Nombo amesema kwa ujumla, mradi unalenga kufikisha mpango wa unywaji wa maziwa shuleni katika jumla ya shule 80 nchini, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamasisha unywaji wa maziwa si kwa watoto pekee bali pia watu wazima huku akisisitiza kuongeza unywaji wa maziwa badala ya soda.


Vilevile Aileen Tinka ambaye ni Afisa mawasiliano kutoka shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN) lenye makao makuu nchini Uswis linalojihusisha na kupambana na utapiamlo na kuboresha lishe duniani,  amesema shirika hilo linafanya kazi kuhakikisha jamii inapata vyakula salama, vya bei nafuu na vyenye virutubishi, huku likilenga zaidi watoto, vijana na wanawake.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Maziwa, Aileen amesema unywaji wa maziwa ya kutosha ni muhimu kwa afya ya watoto na watu wazima, kwani husaidia kuimarisha lishe na kupunguza hatari ya utapiamlo pamoja na magonjwa nyemelezi.

 Pamoja na hayo amesisitiza jamii kuyatambua maziwa kama sehemu muhimu ya chakula cha kila siku na kuahidi kuendelea kushirikiana na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) katika kuhamasisha jamii kuongeza unywaji wa maziwa

Katika namna hiyohiyo Kaimu Mkurugenzi Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) Dr. Dafay Bura amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu bora za mifugo nchini, kwa kuamini kuwa ng’ombe bora anatokana na mbegu bora.

Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuzalisha mbegu bora ili kupunguza utegemezi wa mazao ya mifugo kutoka nje ya nchi na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuimarisha usalama wa chakula.Pia amesema matumizi ya mbegu bora yatawezesha ng’ombe wa asili kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, hivyo kuongeza tija na kipato kwa wafugaji.

Hatahivyo Dr. Bura amewataka watoto kupenda kushiriki katika shughuli za ufugaji na  kuelewa kuwa matumizi ya mbegu bora ni msingi wa mafanikio katika sekta ya mifugo.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652




Post a Comment

Previous Post Next Post