" Dunia kuzalisha umeme wa Nyuklia Mara Tatu ya sasa ifikapo 2060

Dunia kuzalisha umeme wa Nyuklia Mara Tatu ya sasa ifikapo 2060




Uwezo wa kimataifa wa kuzalisha umeme kwa njia ya nyuklia unaweza kuongezeka kwa zaidi ya mara tatu kufikia mwaka 2060, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA), huku nchi mbalimbali zikizidi kuzingatia nishati hiyo kukabili mahitaji yanayoongezeka ya umeme na usalama wa nishati.

Makadirio haya mapya yalitangazwa na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi, wakati wa Mkutano Mkuu wa 70 wa wakala huo unaofanyika mjini Vienna, nchini Austria, ripoti ambayo pia imeeleza kuwa vinu vidogo vya msimu (SMRs) viko mbioni kuwa chanzo kikubwa kipya cha nishati safi sambamba na haja inayoongezeka ya kuchukua nafasi ya vinu vinavyostaafu.

Hii ni mara ya sita mfululizo kwa IAEA kufanya marekebisho ya juu katika makadirio yake ya upanuzi wa nishati ya nyuklia, huku mtazamo huo ukiongezwa kufikia mwaka 2060 katika toleo la mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya nyuma iliyokuwa ikitazama hadi 2050.

Mwishoni mwa mwaka 2025, vinu vya nyuklia 413 vilikuwa vikitumika duniani kote na kutoa gigawati 377.1 za umeme, ambapo katika makadirio ya juu, uwezo huo utafikia gigawati 1,045 ifikapo 2050 na kupanda hadi gigawati 1,284 ifikapo 2060, sawa na takriban mara 3.4 ya kiwango cha 2025, wakati makadirio ya chini yakionyesha ukuaji hadi gigawati 696.

Grossi alisisitiza kuwa uwekezaji katika ujenzi wa vinu vipya na kuongeza muda wa matumizi ya vinu vilivyopo ni mambo ya msingi ili kufikia malengo hayo.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ongezeko kubwa la matumizi ya nishati ya nyuklia linatazamiwa kutokea katika maeneo ya Kati na Mashariki mwa Asia, ambapo uwezo unaweza kupanda kutoka gigawati 114 mwaka 2025 hadi gigawati 407 mwaka 2060 katika makadirio ya juu.

Sambamba na hilo, mchango wa vinu vidogo vya msimu (SMRs) unatazamiwa kupanuka kwa kasi na kufikia asilimia 28 ya uwezo wote mpya wa nyuklia utakaongezwa ifikapo 2060 katika ukuaji wa juu, huku mwelekeo thabiti wa SMRs ukionekana zaidi katika maeneo ya Amerika Kaskazini, Kusini-Mashariki mwa Asia, pamoja na Amerika ya Kusini na Karibea.

Kuhusu suala la vinu vinavyostaafu, ripoti inaonesha kuwa vinu viwili kati ya kila vitatu vya nyuklia vimekuwa vikitumika kwa zaidi ya miaka 30, huku asilimia 45 zikiwa zimefanya kazi kwa zaidi ya miaka 40, jambo linalofanya kuwa muhimu kujiandaa na kuchukua hatua za kufidia kustaafu huko.

Jitihada za kufidia zimeanza kwa baadhi ya vinu kustaafu wakati vingine vipya vikijengwa na kuunganishwa kwenye gridi ya taifa, sanjari na mipango ya ukarabati na sera za kusaidia ushindani wa vinu vya sasa katika masoko huru ya nishati, yote yakiwa ni mwendelezo wa ripoti hiyo ya miaka 46 ya Energy, Electricity and Nuclear Power Estimates for the Period up to 2060 inayotoa mwelekeo wa kina wa kimataifa wa nishati ya nyuklia.

Post a Comment

Previous Post Next Post