" Jukwaa la Uchumi Duniani Latabiri Utulivu wa Uchumi wa Dunia

Jukwaa la Uchumi Duniani Latabiri Utulivu wa Uchumi wa Dunia




Jukwaa la Uchumi Duniani limetoa ripoti ya uchambuzi wa wachumi wakuu wa dunia ambayo inaonesha dalili za kutulia kwa uchumi wa dunia licha changamoto kadhaa zinazojitokeza ikiwamo kuipanda kwa gharama za maisha.

Zaidi ya nusu ya wachumi waliohojiwa, sawa na asilimia 56, wanatarajia uchumi kuwa thabiti au unaoimarika kwa mwaka ujao, ikiwa ni nafuu kubwa ikilinganishwa na mwezi Mei ambapo asilimia 89 walihofu uchumi wa dunia kudhoofika na kuporomoka kabisa.

Licha ya mabadiliko hayo chanya, imani katika utulivu huo bado ni ndogo, huku karibu washiriki wote wakitaja migogoro ya kijiografia kama chanzo kikuu cha kuleta sintofahamu katika utulivu huo unaotabiriwa.

Changamoto nyingine ni kupanda kwa gharama za upatikanaji wa mali na shinikizo katika gharama za maisha.

Hata hivyo asilimia 69 ya wachumi hao wamesema uimara uliouwezesha uchumi wa dunia kuhimili misukosuko mfululizo tangu mwaka 2020 umechochewa kwa kiasi kikubwa na misaada ya fedha kutoka serikalini, huku asilimia 28 pekee ndio wanaotarajia serikali kutoa misaada ya aina hiyo katika mwaka ujao kutokana na kubana kwa bajeti na upungufu wa rasilimali fedha.

Katika uchambuzi, wachumi hao wamekiri kuwa, uimara wa kiuchumi wa siku za usoni utategemea minyororo ya ugavi inayonyumbulika, ubunifu wa kiteknolojia, na mabadiliko ya soko la nishati, huku Marekani na China zikionekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuhimili misukosuko.

Huku matumizi ya akili unde yakiendelea kukua kwa kasi na asilimia 97 ya wataalamu wakitarajia kuongezeka kwa matumizi yake, asilimia 69 wakitarajia faida kubwa za uzalishaji katika kipindi cha miezi 12 ijayo, ukuaji huu wa kiteknolojia unaleta mvutano mkubwa.

Takriban asilimia 79 ya wachumi walihojiwa wamesema wanatarajia upinzani mkubwa kutoka kwa jamii za mitaani dhidi ya upanuzi wa vituo vya data, wakati asilimia 61 hawatarajii miradi hiyo kutengeneza ajira kubwa duniani. Zaidi ya hayo, ujenzi wa vituo vya data unatarajiwa kupandisha bei za umeme na maji katika maeneo husika, wakati mashindano ya akili unde kati ya China na Marekani yakizidi kupungua huku mifumo mikubwa ya lugha ya China ikikaribia kufikia viwango vya wenzao wa Marekani na pengine kupita.

Mgawanyiko wa kijiografia na kiuchumi na utofauti wa kikanda pia vinatarajiwa kuongezeka, huku asilimia 79 ya waliohojiwa wakitarajia vizuizi vya kibiashara na uwezekano wa kuongezeka kwa ushuru nchini Marekani na Ulaya.

Wakati kiasi cha biashara kikitarajia kukua na mauzo ya nje ya China kuelekea masoko yaliyo nje ya Marekani yakiongezeka, matarajio ya ukuaji wa kikanda bado hayako sawa. India, Asia ya Kusini-Mashariki, Asia ya Kati, na Marekani zinapata tathmini thabiti zaidi, wakati Ulaya ikiendelea kubaki nyuma kama eneo dhaifu zaidi. Wakati huohuo, kupanda kwa gharama za chakula, umeme, na usafiri kunatishia kupunguza au kusimamisha mapato halisi ya kaya katika maeneo mengi, jambo ambalo linazifanya serikali kufikiria hatua pana kama vile kupunguza kodi kwa bidhaa muhimu, kutoa ruzuku za matumizi, na kudhibiti bei.

Post a Comment

Previous Post Next Post