" Kambole: Usiri na Pengo la Taarifa Vinafuga Uvumi

Kambole: Usiri na Pengo la Taarifa Vinafuga Uvumi




Mwanasheria na Wakili Mkuu kutoka Law Guards Advocates, Adv. Jebra Cunbert Kambole, amesema uadilifu ndio ajenda chanya, kufanikisha upatikanaji wa taarifa na wala si udhibiti.

Aidha amesema watu hawawezi kuamini, kufuatilia au kupima taarifa ambazo hawaruhusiwi kuziona na kuonya dhidi ya kuifanya serikali au jamii kuishi katika lindi la giza la taarifa.

Kambole alisema hayo katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa (IDUAI 2026), wakati akiwasilisha tathmini tunduizi kuhusu hali halisi ya upatikanaji wa taarifa nchini Tanzania kuanzia Septemba 2025 hadi Septemba 2026.

Akizungumzia umuhimu wa kulinda uadilifu wa taarifa katika enzi za kidijitali na jinsi upatikanaji wa taarifa unavyoweza kusaidia kukabili changamoto za upotoshaji wa habari, alisisitiza kuwa ukosefu wa taarifa rasmi ni mbolea inayochochea machafuko ya taarifa na uvumi unaoenea kwa kasi.

Katika kufafanua mfumo huu, alisema kuwa "pengo la taarifa linaendelea kujazwa na uvumi na ukweli uliopotoshwa," hali inayowafanya wananchi kukosa chanzo cha kuaminika na hatimaye kujikuta wakitumbukia kwenye makosa ya kisheria pale wanapojaribu kutafuta au kusambaza ukweli.

Mtoa mada alibainisha kuwepo kwa mianya ya kisheria na utamaduni wa usiri unaoleta madhara makubwa kwa ustawi wa taarifa sahihi, akisisitiza kuwa "sheria za usiri zinatawala juu ya haki ya kujua," jambo ambalo linasababisha vyombo vya serikali kujifungia na kuacha nafasi kubwa ya uvumi.










Kuhusu upande wa mahitaji na matumizi ya habari kwa wananchi, vyombo vya habari, na mashirika ya kiraia, tathmini hiyo ilionyesha kuwa mzigo mkubwa unaangukia kwa raia badala ya wajibu wa taasisi za umma kutoa habari kwa hiari.

Adv. Kambole alitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua saba za dhati ili kujenga mustakabali ulio wazi na wa kuaminika zaidi.

Miongoni mwa hatua hizo saba ni kukuza elimu ya matumizi ya vyombo vya habari na habari za kidijitali (media and information literacy), kuanzisha tovuti za umma kwa lugha ya Kiswahili, kuimarisha mtandao wa kukagua ukweli (fact-checking), na kuweka mifumo salama ya kuwalinda wanahabari.

Hatua nyingine ni kuundwa kwa daftari au rejista ya wazi ya vizuizi vyote (public register of restrictions), ambapo kila hatua ya kufungwa kwa mitandao, kusimamishwa kwa vyombo vya habari, au kuchukuliwa kwa hatua za kiudhibiti iwekwe wazi pamoja na sababu zake na njia za kisheria za kukata rufaa.

Post a Comment

Previous Post Next Post