Kampuni kubwa kutoka nchini Japan zinatarajia kufanya ziara rasmi nchini mwezi Machi 2027 kwa lengo la kutathmini fursa za uwekezaji na kukuza uzalishaji wa ndani, ikiwa ni matokeo ya mazungumzo yaliyofanywa na ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokutana na viongozi wa Shirikisho la Sekta Binafsi la Japan na taasisi mbalimbali nchini humo.
Akieleza malengo ya ziara hiyo, Profesa Kitila alisema inalenga kubadili mfumo wa biashara uliopo ambapo kwa sasa Japan huuza bidhaa nyingi zaidi nchini Tanzania kuliko Tanzania inavyouza huko, ambapo serikali inataka kampuni hizo kuja kuwekeza na kutengeneza bidhaa hizo hapa nchini, zikiwemo mashine na bidhaa za kilimo, badala ya kuendelea kuwa soko la kuagiza bidhaa kutoka nje.
Alibainisha kuwa sehemu kubwa ya bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka Japan ni pamoja na magari, hivyo serikali inalenga kuvutia uwekezaji wa uzalishaji wa vyombo hivyo na bidhaa nyingine ili kuongeza ajira, matumizi ya teknolojia, na kuboresha uwiano wa biashara ambao ulifikia Dola za Marekani milioni 622.3 mwaka 2024 sawa na Bilioni 94.27 za Yen.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania ulikutana pia na Shirika la Biashara ya Nje la Japan (JETRO) na kukubaliana kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), sambamba na kufanya mazungumzo na wizara mbalimbali za Japan kuhusu miundombinu, biashara, na kuandaa Mkataba wa Makubaliano (MoU) utakaotekelezwa kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA).
Profesa Kitila aliongeza kuwa ziara hiyo itafungua pia fursa za ushirikiano wa kiuchumi na utalii kati ya Zanzibar na Okinawa kutokana na kufanana kwa maeneo hayo mawili katika utalii na fukwe, huku hatua hii ikija wakati Tanzania na Japan zikitimiza miaka 60 ya uhusiano ambapo mwelekeo sasa ukitoka kwenye misaada na kuelekezwa kwenye biashara na uwekezaji ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment