" Kihongosi Awataka Wananchi Kulinda Amani na Kuwakataa Wanasiasa Wanaohamasisha Vurugu

Kihongosi Awataka Wananchi Kulinda Amani na Kuwakataa Wanasiasa Wanaohamasisha Vurugu




Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amewasihi wananchi kusimama imara katika kulinda amani ya nchi na kuwakataa wanasiasa wote wanaojaribu kuhamasisha vurugu, akionya kuwa kupotea kwa amani kutavuruga shughuli za kila siku na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Akizungumza hivi karibuni katika Kata ya Manza, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, wakati akizindua Shina Namba Sita katika Kijiji cha Mbuyuni ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili ya kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025 hadi 2030, Kihongosi alieleza kuwa amani ndiyo ngao inayowawezesha wananchi kuabudu, kufanya biashara, na kushiriki shughuli za kijamii na michezo bila hofu, hivyo hakuna anayepaswa kuruhusiwa kuihatarisha.

Katika ziara hiyo iliyobeba pia ajenda za maendeleo na uimarishaji wa miundombinu ya chama, Kihongosi alikagua na kuzindua nyumba nne za watumishi wa CCM na jumuiya zake wilayani Mkinga, ambazo ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 36 zinazotekelezwa katika wilaya tisa za kichama mkoani Tanga kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5.

Alibainisha kuwa utekelezaji huo wa miradi ya kimkakati unathibitisha uthabiti wa chama chake ikilinganishwa na vyama vya upinzani ambavyo vimeshindwa kufanya vizuri kutokana na changamoto za uongozi na ukosefu wa rasilimali fedha, huku akimpongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahman, kwa kuimarisha uhai wa chama na kudumisha ushirikiano mzuri na serikali.

Akigusia changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo, kiongozi huyo alitambua tatizo sugu la maji linaloisibu Wilaya ya Mkinga na kueleza kuwa serikali imeweka mikakati thabiti kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 35 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaotatua kero hiyo ya muda mrefu na kuwaletea wananchi unafuu mkubwa katika maisha yao ya kila siku.

Post a Comment

Previous Post Next Post