" NGAYIWA: MIRADI ILIYOKWAMA YAKWAMULIWA NDANI YA MIEZI TISA

NGAYIWA: MIRADI ILIYOKWAMA YAKWAMULIWA NDANI YA MIEZI TISA





Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema ndani ya miezi tisa tangu viongozi wachaguliwe, Serikali imeanza kutekeleza kwa kasi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwemo kufufua na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu katika maeneo ya Kahama.

Ngayiwa amesema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa barabara za lami ndani ya Mji wa Kahama kupitia mradi wa TACTIC, ambao kwa muda ulikuwa umekwama, lakini sasa mkandarasi ameshaanza kazi baada ya kupewa mkataba wa miezi saba unaotarajiwa kukamilika Januari 2027.

“Mradi wa barabara ulikuwa umekwama na sasa hivi ameshaanza, sote ni mashahidi na ninyi mashahidi, naona mradi huo unaenda,” amesema Ngayiwa.

Amesema Serikali pia imechukua hatua kukabiliana na ajali zilizokuwa zikitokea katika eneo la Lumambo, barabara ya kuelekea zongomera, kwa kuweka taa za kuongozea magari, hatua ambayo amesema imepunguza kwa kiasi kikubwa ajali katika eneo hilo.

Katika sekta ya maji, Ngayiwa amesema ujenzi wa tangi
la maji eneo la Shunu-Rugera, ambao ulikuwa umekwama, sasa umekamilika na maji yameanza kupatikana, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuendelea kuyasambaza kwa wananchi wa Rugera.

Amesema Serikali pia inaendelea kutekeleza mradi wa chujio la Buzwaga, ambao ukikamilika utasaidia kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji na kupunguza tatizo la kukatika kwa huduma.

Ngayiwa amesema hivi karibuni kulikuwa na changamoto ya maji kwa siku kadhaa, lakini kukamilika kwa miradi hiyo kutasaidia kuhakikisha maji yanapatikana, yanasukumwa kwenye matenki na kuendelea kusambazwa kwa wananchi.

Katika afya, amesema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika hospitali ya Manispaa ya Kahama, ambalo litakapokamilika litaboresha huduma kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga.

Amesema pia hospitali hiyo sasa ina mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni, hatua itakayosaidia wagonjwa wenye changamoto za upumuaji pamoja na wanaolazwa katika vyumba vya uangalizi maalum (ICU) kupata oksijeni bila kutegemea kununua mitungi kutoka hospitali nyingine.

Post a Comment

Previous Post Next Post