" SDA wapongeza serikali kwa kuimarisha amani, maendeleo

SDA wapongeza serikali kwa kuimarisha amani, maendeleo




Mwenyekiti wa Majengo, Kanisa la Waadventista wa Sabato Salasala (SDA),Bw. Charles Wangwe ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha, kulinda na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano na mahusiano mema miongoni mwa Watanzania wa makundi ya imani mbalimbali katika Taifa letu.

Alisema hayo wakati akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi, katika harambee ya kuchangia ujenzi na maendeleo ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA), Salasala, jijini Dar es Salaam leo, Septemba 26, 2026.

Alisema kutokana na juhudi za serikali kumekuwepo na amani na ushirikiano unaowezesha shughuli mbaliombali za kijamii kama kuabudu na kiuchumi kuendelea kutendeka bila hofu.

Akilizungumzia kanisa hilo, amesema Kanisa la Waadventista wa Sabato lililoanzishwa mwaka 2007 likiwa na washiriki wachache; mwaka 2010 washiriki walifika 150, mwaka 2018 waumini 400 na wengine kukaa nje, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa ujenzi wa jengo kubwa lenye uwezo wa kuchukua watu 1,500 na kukadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 3.

Ameendelea kwa kusema kuwa kanisa linaendesha hospitali, kliniki, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Zahanati ya Pemba, vituo 12 vya afya, ambazo ni zahanati 11 na polyclinic moja.

Sambamba na hayo, Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa likichangia katika maendeleo ya elimu, ambapo jumla ya shule 27 za awali, 23 za msingi, 18 za sekondari, Chuo kimoja cha VETA, Chuo kimoja cha Afya na Chuo kimoja cha kati kilichopo Dodoma.










Naye Naibu Waziri Dkt. Evaline Munisi, amelipongeza Kanisa la Waadventista wa Sabato Salasala (SDA) kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mshikamano wa kijamii, kukuza maadili ya uadilifu, uwajibikaji na upendo, pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na mshikamano wa kitaifa.

Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imejipanga kushirikiana na makundi ya kijamii katika kudumisha mshikamano, kukuza ustahimilivu, kuimarisha maadili ya kazi na kusaidia jitihada za kijamii na maendeleo endelevu.

Kadhalika, Dkt. Munisi amewapongeza viongozi na waumini wa Kanisa la SDA Salasala kwa kuandaa harambee hii ya ujenzi wa kanisa yenye lengo la kukusanya Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga jamii imara.

“Tusimame pamoja, tutoe kwa moyo wa furaha, tutashuhudia Kanisa la Waadventista wa Sabato linajengwa na kudumishwa imara kwa utukufu wa Mungu,” amesema Dkt. Munisi.

Vilevile, Dkt. Munisi amewasihi viongozi na waumini wa kanisa kuendelea kuyaenzi na kuimarisha mafundisho ya kiroho na malezi ya watoto na vijana, umoja, upendo na mshikamano, ushirikiano na Serikali, pamoja na kuwa na uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za kanisa.

Post a Comment

Previous Post Next Post