" KONGAMANO LA UFUATILIAJI NA TATHMINI ARUSHA, USHAHIDI KWENDA VITENDO.

KONGAMANO LA UFUATILIAJI NA TATHMINI ARUSHA, USHAHIDI KWENDA VITENDO.

 


Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.

Kongamano la tano la Ufuatiliaji na Tathmini linatarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2026, likiwa na lengo la kuwakutanisha viongozi na watendaji mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, tathmini na ujifunzaji katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

 Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla amesema  Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu.

Amesema kuwa Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza, litatoa fursa kwa washiriki kubadilishana mbinu, uzoefu na maarifa yanayohusiana na ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo. 

Pia CPA Makalla amesema litasaidia kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna bora ya kutumia matokeo ya ufuatiliaji katika kuboresha utekelezaji wa mipango mbalimbali.

Kauli mbiu ya kongamano hilo ni “Kutoka katika Ushahidi Kwenda Vitendo”, ikilenga kuhakikisha kuwa taarifa na ushahidi unaopatikana kupitia mifumo ya ufuatiliaji na tathmini unatumika katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua zinazolenga kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Kongamano hilo pia linalenga kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ajenda ya Afrika 2063 pamoja na mikataba na makubaliano mengine ya kimkakati.

Vilevile amefafanua kuwa Washiriki wanatarajiwa kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa katika nyaraka hizo yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayopimika.

CPA Makalla amesema"Hatua hiyo inalenga pia kuunga mkono azma ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora na kupata ufumbuzi wa kero zinazowakabili,  miongoni mwa maeneo yanayolengwa ni upatikanaji wa huduma bora za afya, maji, elimu na huduma nyingine muhimu, huku ufuatiliaji na tathmini ukitumika kuhakikisha utekelezaji wa mipango hiyo unaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi"

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali, Charlton Meena, amesema kongamano hilo linakuja wakati ambapo Tanzania imehitimisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya miaka mitano, hivyo sasa ni wakati wa kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Amesema hatua hiyo inahitaji kuweka misingi imara ya utawala wa sera na kiutendaji, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha mipango na sera zinazowekwa zinatafsiriwa kuwa matokeo halisi yanayowanufaisha wananchi.

Meena amesema zaidi ya washiriki 1,500 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo, huku mada mbalimbali zitakazojadiliwa zikilenga kauli mbiu ya “Kutoka katika Ushahidi Kwenda Vitendo”, kwa kuangalia namna ushahidi na taarifa zinazopatikana kupitia ufuatiliaji na tathmini zinavyoweza kutumika kuboresha maisha ya wananchi na kufanikisha maendeleo endelevu.

Hata hivyo ameongeza kuwa,  kongamano hilo litajadili pia mbinu bora za matumizi ya takwimu katika ufuatiliaji na tathmini, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi zitakazosaidia Serikali kufanya maamuzi yenye tija na kuweka mikakati inayolenga kutatua changamoto na kuboresha huduma kwa wananchi.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652

Post a Comment

Previous Post Next Post