" KONGAMANO LA UFUATILIAJI NA TATHMINI LAWEKA MAAZIMIO YA KUTEKELEZA DIRA 2050

KONGAMANO LA UFUATILIAJI NA TATHMINI LAWEKA MAAZIMIO YA KUTEKELEZA DIRA 2050



Na, Egidia Vedasto, 

Misalaba Media, Arusha.

Kongamano la Tano la Ufuatiliaji na Tathmini na kujifunza  limefungwa kwa kuweka maazimio ya kimkakati yanayolenga kusaidia kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Akifunga kongamano hilo, Jijini Arusha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mwinyi Ahmed Mwinyi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Profesa Paramagamba Kabudi, amesema zaidi ya mada 36 zilizowasilishwa katika kongamano hilo zimejadiliwa kwa kina.

Amesema washiriki wanapaswa kutumia maarifa na uzoefu walioupata katika kongamano hilo katika maeneo yao ya kazi, ili kuhakikisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini inatumika ipasavyo katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Aidha, amesema taifa linapoanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, mafanikio yake yatapimwa kwa kuangalia maendeleo na mabadiliko yanayotokea katika maisha ya wananchi.

Mwinyi amesema "Ushahidi unapaswa kuwa msingi wa maamuzi, huku mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ikitumika kama mfumo wa kutoa tahadhari za mapema.Kila taasisi itumie mifumo hiyo kwa kuzingatia muktadha wake,  teknolojia mpya zikitumike kwa uangalifu na ubora wa maamuzi kutegemea ubora wa ushahidi unaopatikana".

Katika namna hiyohiyo amesema vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wanapaswa kushirikishwa katika maamuzi yanayowahusu.

Hata hivyo amesisitiza Ofisi ya Waziri Mkuu  kuharakisha sera ya ufuatiliaji na tathmini, kuimarisha ushirikiano na Ofisi ya Utumishi, pamoja na kuhakikisha vitengo vya ufuatiliaji na tathmini vina wataalamu wenye sifa. Taasisi za ufuatiliaji katika halmashauri, mikoa na Serikali za Mitaa pia zimetakiwa kuimarisha kliniki za uwajibikaji.


Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, amewashukuru wadhamini wa kongamano hilo pamoja na washiriki takribani 1,664 kutoka ndani na nje ya nchi kwa kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo.

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 unahitaji umakini na ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuhakikisha unaleta matokeo jumuishi na kuongeza tija katika maendeleo ya taifa.

Dkt. Yonazi amesema ufuatiliaji na tathmini ni muhimu katika kuhakikisha mipango na sera za Serikali zinatekelezwa kwa ufanisi, huku takwimu na ushahidi vikitumika katika kufanya maamuzi sahihi na kuratibu shughuli za maendeleo.

Amesema Serikali itazingatia maazimio yote yaliyofikiwa katika kongamano hilo, pamoja na maazimio mengine yatakayoongezwa, ili kuwezesha uratibu mzuri wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini.

Katika maazimio 10 yaliyosomwa na Dkt. Rodgers Rumenyela kutoka Chama cha wataalam wa ufuatiliaji na tathmini nchini TANEA mbele ya mgeni rasmi, amesema maazimio hayo yameweka msingi wa kufikia mafanikio yenye tija kwa wananchi, huku vijana wakipewa kipaumbele katika fursa za kujifunza kwa vitendo.

Amesema taasisi zinapaswa kuweka mazingira wezeshi kwa matumizi ya akili mnemba, huku Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu ikitakiwa kuongeza uelewa na kusimamia masuala ya tathmini ili kuimarisha matumizi ya ushahidi katika maendeleo.

Maazimio hayo pia yameitaka Serikali kuimarisha mbinu na miongozo ya ufuatiliaji na kuhakikisha maafisa masuuli wanashirikiana katika ngazi zote kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini. 

Dkt.Rumenyela amesema , mfumo jumuishi wa kitaifa wa kielektroniki unatakiwa kukamilishwa na kuunganishwa na mifumo iliyopo kwa ajili ya kukusanya taarifa.

Ameongeza kuwa  maazimio mengine ni kukamilisha Sera ya Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na mkakati wake, huku taasisi zote za umma zikitakiwa kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za ufuatiliaji ili kuhakikisha mipango na miradi inatekelezwa na kufikia malengo yaliyowekwa.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652


Post a Comment

Previous Post Next Post