Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.
Ziwa Duluti Laitwa Kivutio cha Kizazi Hadi Kizazi
Naibu Waziri wa Utalii, Hamad Hassan Chande, amepongeza uwepo wa utalii wa maombi katika Hifadhi ya Msitu wa Ziwa Duluti, akisema aina hiyo ya utalii ina umuhimu katika kukuza imani za watu na kuchangia maendeleo endelevu ya eneo hilo.
Chande amesema uwepo wa Ziwa Duluti na mazingira yake ya asili unatoa fursa kubwa ya kuendeleza utalii wa aina mbalimbali, ikiwemo utalii wa maombi, hivyo ni muhimu kuendelea kutunza mazingira na vivutio vilivyopo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuongeza wigo wa uwekezaji katika eneo hilo, hususan katika kuboresha miundombinu na huduma za utalii, ili kuvutia watalii wengi zaidi na kuongeza mchango wa eneo hilo katika uchumi wa taifa.
“Ziwa hili halikauki na litakuwa kivutio kwa kizazi hadi kizazi,” amesema Chande, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii katika kulinda na kuendeleza Ziwa Duluti kama kivutio muhimu cha utalii.
Katika namna hiyohiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Korogwe vijijini Timotheo Mzava, ameongoza wajumbe wa Kamati hiyo katika ziara ya kutembelea Hifadhi ya Msitu wa Ziwa Duluti, Wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Ziara hiyo imelenga kujionea hali ya uhifadhi wa eneo hilo, kutathmini fursa zinazotokana na utalii wa ikolojia pamoja na kujadili changamoto zinazokabili usimamizi na uhifadhi wa Hifadhi ya Msitu wa Ziwa Duluti.
Mzava amepongeza kazi kubwa inayofanywa na sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya utalii nchini, akieleza kuwa mchango wao ni muhimu katika kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha huduma kwa watalii.
"Natoa wito kwa Watanzania kutembelea na kuvifahamu zaidi vivutio vya utalii vilivyopo nchini, nakaribisha sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika Hifadhi hii hususan katika kuboresha miundombinu na huduma, kuelekea maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027" Amesema.
Katika namna hiyohiyo Mhifadhi Mkuu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Peter Myonga, ameshukuru uongozi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kutembelea Hifadhi ya Msitu wa Ziwa Duluti, akisema ziara hiyo ni muhimu katika kutambua fursa zilizopo na kuendelea kuhamasisha utalii wa ndani.
Myonga amesema TFS imeendelea kujiandaa kuelekea mashindano ya AFCON 2027 kwa kuboresha huduma na miundombinu katika hifadhi hiyo, ikiwemo kujenga na kuongeza maeneo ya malazi ili kuwa na uwezo wa kuhudumia wageni wengi zaidi watakaotembelea eneo hilo wakati wa mashindano hayo.
Ametaja baadhi ya vivutio vinavyopatikana katika Hifadhi ya Msitu wa Ziwa Duluti kuwa ni utalii wa maombi, kutembea ndani ya ziwa, matembezi ya kitalii katika hifadhi hiyo, pamoja, fursa ya kushuhudia mandhari ya vilele vya Mlima Meru na Kilimanjaro na kumuona Mnyama Kenge.
"Makundi mbalimbali yamekuwa yakitembelea hifadhi hii, yakiwemo wasanii, wanakwaya na wanaharusi, natoa wito kwa jamii kuendelea kutembelea Ziwa Duluti ili kujionea na kufurahia vivutio vilivyopo, kuongezeka kwa watalii wa ndani kutasaidia kukuza utalii, kuongeza mapato ya Serikali na kuchangia uhifadhi wa mazingira" Amesema
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
.
Post a Comment