Kufuatia maagizo ya wazi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka Jiji la Dar es Salaam kuwa safi na salama, kikosi kazi maalum cha usimamizi wa Sheria Ndogo ya Afya, Usafi na Usimamizi wa Mazingira imewakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria zaidi ya watu 500 waliokiuka taratibu za utunzaji wa mazingira jijini humo.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi kubwa la usafi wa mazingira wilayani Ilala, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, ameweka wazi kuwa katika zoezi hilo lililowagusa wakazi zaidi ya milioni sita wa wilaya hiyo, watu 340 walipatiwa maonyo rasmi, huku watu 19 wakilipa faini za papo hapo kuanzia shilingi laki tatu hadi milioni moja kwa makosa ya uchafuzi wa mazingira, wakati watu 121 walifikishwa moja kwa moja mahakamani ambapo 51 kati yao wamehukumiwa vifungo vya kuanzia miezi 12 hadi 24 ili iwe fundisho kwa wote wenye tabia ya kutupa taka ovyo.
Hatua hii ya kuwakamata na kuwahukumu wahalifu wa mazingira inakwenda sambamba na mkakati thabiti wa Jiji wa kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa bila huruma, ambapo kupitia Kifungu cha 41 cha Sheria Ndogo ya Afya, Usafi na Usimamizi wa Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya mwaka 2024, mamlaka zimejipanga kusimamia nidhamu ya usafi mtaa kwa mtaa kwa kushirikiana na askari 50 wa Jeshi la Akiba waliopatiwa mafunzo maalum katika Ukumbi wa Karimjee chini ya usimamizi wa Kaimu Mkurugenzi na Mwanasheria Mkuu wa Jiji, Faraja Nakua.
Askari hao wapya wameelekezwa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kuzingatia haki za wananchi bila kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa, huku wakisimamia makosa yote ikiwemo utupaji wa taka hovyo, uchafuzi wa vyanzo vya maji, uchomaji wa taka unaosababisha uchafuzi wa hewa, ukataji miti holela, na uzibaji wa mifereji inayosaidia kuzuia mafuriko.
Aidha ufuatriliaji wa sheria hii ndogo umeonesha mafanikio makubwa katika sekta ya usafiri wa umma, ambapo asilimia 99 ya daladala zimeshaanza kufuata agizo la kuwa na vyombo vya kuhifadhia taka ndani ya magari yao.
Sambamba na hatua hizo kali za kisheria, hivi karibuni uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, umezidi kukaza kamba kwa kutoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wadogo wanaofanya shughuli zao mbele ya maduka, barabarani, na kwenye mifereji ya maji eneo la Kariakoo kuondoa biashara hizo na kuhamia maeneo rasmi yaliyotengwa, lengo likiwa ni kurejesha utaratibu, kurahisisha usafishaji wa mitaro, na kuzuia maji kutiririka hovyo mitaani.
Vilevile, wafanyabiashara wote wametakiwa kuwa na mapipa ya taka (dustbins) katika maeneo yao ya biashara huku wakisisitizwa kutunza miundombinu hiyo.
Serikali ya wilaya na mkoa imesisitiza kuwa haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote watakaokaidi maagizo haya, kwani jitihada hizi zote zinalenga kujenga utamaduni wa kudumu wa uwajibikaji ili kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa kivutio safi, salama, na lenye mazingira bora yanayoendana na hadhi ya nchi.
PROFESSOR MGOKO EPISODE 03
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment