" SANGU AZUNGUMZA NA JUMUIYA YA AHMADYYA ATAKA TAASISI ZA DINI KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO

SANGU AZUNGUMZA NA JUMUIYA YA AHMADYYA ATAKA TAASISI ZA DINI KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amezitaka Taasisi za Dini nchini kuendeleza ushirikiano na Serikali katika kudumisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Mhe. Sangu amesema hayo leo Septemba 26, 2026, alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka (Jalsa Salana) wa 55 wa Jumuiya hiyo, uliofanyika Msongola, Dar es Salaam.

Amesema, Serikali inatambua mchango wa Jumuiya ya Ahmadiyya na taasisi nyingine za dini katika kuimarisha mahusiano ya kijamii, malezi ya watoto na vijana, pamoja na kutoa huduma katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii.

Aidha, amewataka waumini kuendelea kuenzi kaulimbiu ya mkutano huo, “Taqwa (Ucha Mungu) Ndiyo Mzizi wa Kila Wema,” akisema inapaswa kuwa msingi wa kuhimiza maadili, kuheshimu wazazi na walezi, kupinga ukatili dhidi ya watoto na kuwaelekeza vijana kuepuka dawa za kulevya na matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii.














Vilevile, amepongeza Jumuiya hiyo kwa kuandaa mkutano huo wa kikatiba na kusisitiza kuwa mikutano ya aina hiyo inatoa nafasi kwa wanachama kujadili masuala ya taasisi na kuchangia ukuaji wake. Alisema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na makundi ya kijamii, ikiwemo taasisi za dini, katika kuimarisha ushirikishwaji, uwajibikaji na mshikamano wa kitaifa.

Kwa upande wake, Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad, aliishukuru Serikali kwa kushiriki katika mkutano huo, akisema uwepo wa viongozi wa Serikali unaakisi mahusiano mazuri kati ya Serikali na jamii. Aliahidi kuendeleza ushirikiano huo na kuendelea kutekeleza malengo ya Jumuiya kwa manufaa ya jamii na Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post