" TANZANIA, MISRI ZAAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA NA KIUCHUMI

TANZANIA, MISRI ZAAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA NA KIUCHUMI




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania na Misri zimedhamiria kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi hizo katika sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, elimu, afya na masuala ya kimataifa.

Waziri Kombo amesema hayo jijini New York, nchini Marekani, katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mhe. Dkt. Badr Abdelatty, yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza wigo wa biashara na uwekezaji.

Katika kuimarisha uchumi, alibainisha kuwa Misri tayari ina miradi 61 ya uwekezaji nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5, ambayo inatekelezwa katika sekta mbalimbali na imetoa ajira 5,364.

Waziri Kombo aliongeza kuwa Tanzania inathamini sana mchango wa kampuni za Misri katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, hususan Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 uliotekelezwa na kampuni za nchi hiyo na kuzinduliwa rasmi Agosti 22, 2026.

Mbali na miundombinu, nchi hizi mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kijamii zikiwemo elimu, afya, kilimo, maji na teknolojia, ambapo Misri imeahidi kutoa nafasi 10 za ufadhili wa masomo kupitia Samia Scholarship, sambamba na zaidi ya Watanzania 420 wenye matatizo makubwa ya moyo kunufaika na huduma za upasuaji kupitia kambi za madaktari bingwa kutoka Misri hapa nchini.

Kwa upande wake, Mhe. Abdelatty alisisitiza dhamira thabiti ya nchi yake ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kidiplomasia kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili.

Post a Comment

Previous Post Next Post