" TAASISI ZA KIDINI ZAELEZWA KUWA NGUZO MUHIMU YA AMANI NA UTULIVU WA TAIFA

TAASISI ZA KIDINI ZAELEZWA KUWA NGUZO MUHIMU YA AMANI NA UTULIVU WA TAIFA




Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema Serikali haiwezi kufanikisha maendeleo bila ushirikiano na taasisi za dini, akieleza kuwa taasisi hizo ni nguzo muhimu ya amani, utulivu na ustawi wa Taifa.

Sangu amesema hayo katika harambee ya ujenzi wa nyumba za mapadre wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Kijiji cha Matai, Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.

Ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa kugharimu Sh milioni 93, huku harambee hiyo ikifanikiwa kukusanya Sh milioni 25.9, ambapo Sangu amechangia Sh milioni 10.

Waziri Sangu ameipongeza Parokia ya Matai kwa kufanikisha ujenzi wa kanisa la parokia hiyo, akisema hatua hiyo ni mfano wa mshikamano wa waumini na jamii katika kuchangia maendeleo ya kiroho na kijamii.

Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Leonardo Nkungwe, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wake na taasisi za dini katika kuleta maendeleo na ustawi wa jamii.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Peter Lijualikali, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa waumini na jamii katika kufanikisha miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni chachu ya mafanikio ya miradi ya kijamii na kiroho.

Awali, akisoma risala kwa niaba ya Parokia ya Matai, Diwani wa Kata ya Mkowe, Chrispin Mwananyau, amesema waumini na jamii wamejitoa kwa dhati katika ujenzi wa kanisa la parokia hiyo, mradi uliogharimu Sh milioni 250, na sasa wanaendelea kushirikiana katika ujenzi wa nyumba za mapadre.

Post a Comment

Previous Post Next Post