Na Edington Ezron, Misalaba Media
Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Shinyanga
wameiomba serikali na mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kuhusu tahadhari
zinazopaswa kuchukuliwa kuelekea msimu wa mvua zinazotarajiwa kuwa na athari
kwa makazi ya watu, mifugo na maisha ya wananchi.
Wananchi hao kutoka katika mitaa mbalimbali ya
Manispaa ya Shinyanga wameyasema hayo kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza
na Misalaba Media, ambapo wameeleza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema ili
kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
Mmoja wa wananchi hao, Elias Masanja, amesema kila
mwananchi anapaswa kuchukua hatua za kujikinga na athari za mvua hizo hususani
kwa wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabonde.
Kwa upande wake, Michael Peter amesema wananchi
hawapaswi kupuuza taarifa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), akisema baadhi ya watu wamekuwa wakizichukulia taarifa hizo
kama jambo la kawaida, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa.
Aidha, wananchi hao wameiomba serikali kushirikiana
nao katika kuboresha miundombinu ya kupitisha maji, ikiwemo ujenzi wa mifereji
na mitaro, ili kupunguza hatari ya mafuriko katika makazi ya watu.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Miti Mirefu, Nassoro
Warioba, amesema wameanza mchakato wa kuzibua mitaro katika baadhi ya maeneo ya
mtaa huo, huku wakiendelea na jitihada za kurekebisha maeneo yenye changamoto,
ikiwemo karavati lililopo katika barabara ya Mwanza–Mkabara na Shy Pazuri.
Warioba ameongeza kuwa serikali ya mtaa inaendelea
kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, ikiwemo maeneo ya
Mto Buluba na maeneo mengine yenye changamoto.
Amewasihi wananchi kuchukua hatua za mapema, ikiwemo
kuziba madimbwi ya maji, ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko na
madhara mengine yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwinamila, Juma
Athuman Mboma, amewasihi wananchi kuzingatia usalama wao wakati wa mvua,
ikiwemo kuepuka kutembea wakati mvua kubwa inanyesha ili kujikinga na hatari ya
kupigwa na radi au kusombwa na maji.
Pia ameiomba serikali kupitia Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) kutoa ushirikiano kwa wananchi kwa kujenga mitaro
ya kupitisha maji na kuyaelekeza katika maeneo salama yasiyo na makazi ya watu.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa
tahadhari kwa wananchi kuhusu uwezekano wa mvua kubwa katika kipindi kijacho,
huku ikiwataka kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua
tahadhari mapema ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza, ikiwemo
mafuriko, upepo mkali na radi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment