" Wanasayansi Wagundua Sayari Inayozunguka Nyota Yake kwa Mwelekeo wa Kinyume

Wanasayansi Wagundua Sayari Inayozunguka Nyota Yake kwa Mwelekeo wa Kinyume




SEPTEMBA 21,2026 wanasayansi walichapisha ugunduzi kwenye jarida la kisayansi la Astronomy & Astrophysics ambao umekuwa na maswali mengi kuhusu kukiukwa kwa sheria za asili za anga za juu kwa kuwepo sayari inayokwenda kinyume kanuni hizo.

Sayari hiyo iliyojadiliwa ipo anga za mbali, kiasi cha miaka 73 ya miaka.Kwa mujibu wa chapisho hilo, sayari hiyo inakwenda kinyume na nyota yake wakati ikijizungusha yenyewe.

Umbali wa miaka ya mwanga 73 ni mkubwa sana yaani katika hesabu mwaka mmoja wa mwanga ni kipimo cha mwanga unaposafiri katika kipindi cha mwaka mmoja sawa na takriban kilometa trilioni 9.46, na ukizidisha kwa miaka hiyo 73 unapata takriban kilometa trilioni 690.

Kwa upande wa muda wa kusafiri, ikiwa chombo kingeweza kusafiri moja kwa moja kwa kasi ya mwanga, ambambo kwa teknolojia ya sasa ya kibinadamu bado haiwezekani, ingechukua miaka 73 kamili kufika huko.

Hata hivyo, kwa kutumia teknolojia ya sasa ya vyombo vya anga za juu vinavyosafiri kwa kasi ya kawaida ya makumi ya kilometa kwa sekunde, safari ya kwenda huko ingechukua mamilioni ya miaka, hapa tunazungumzia zaidi ya miaka milioni moja.

Kwa vyombo kama Voyager huchukua makadirio ya miaka 70,000 hadi 80,000 kusafiri umbali wa mwaka mmoja tu wa mwanga.

Sayari hiyo iliyopo nje ya mfumo wetu wa jua (exoplanet), inatambulika kwa jina la GJ 3090 b na ipo umbali wa miaka ya mwanga takriban 73 kutoka duniani, ina mzunguko uliopinda kwa kiasi kikubwa sana kiasi kwamba inazunguka kwa mtindo wa kurudi nyuma (retrograde orbit).

Jambo hili limewashangaza sana watafiti kwa sababu, kulingana na misingi ya sayansi ya anga, sayari huundwa kutoka kwenye diski za gesi na vumbi zinazozunguka nyota changa, jambo ambalo linapaswa kuzifanya sayari hizo zote zizunguke katika mwelekeo mmoja na kwenye mhimili unaofanana na wa nyota mama.

Mjumbe wa timu ya utafiti, Yann Carteret kutoka Idara ya Unajimu ya Chuo Kikuu cha Geneva (UNIGE), ameeleza kuwa kwa mshangao mkubwa, si tu kwamba sayari hii ina mzunguko uliopinda vibaya, bali pia inazunguka kinyume kabisa na mwelekeo wa nyota yake.

Ili kupima tofauti ya mwelekeo kati ya mhimili wa nyota na mzunguko wa sayari yake, wanasayansi hutumia kipimo kinachoitwa pembe ya Psi, ambapo kwa mfano duniani pembe hiyo ni ndogo sana ya digrii 7 tu.

Hata hivyo, walipochunguza sayari hii yenye ukubwa unaofikia mara 2.2 ya Dunia na uzito wa mara 4.5 ya sayari yetu (aina ya sayari inayofahamika kama "sub-Neptune") kwa kutumia kifaa cha kisasa cha NIRPS kilichoko katika Kituo cha Uangalizi cha La Silla, waligundua kuwa GJ 3090 b ina pembe ya Psi inayofikia digrii 136; na hii inashangaza.

Hali hii inafanya mfumo huu kuwa miongoni mwa mifumo mitano tu kuwahi kushuhudiwa kote angani yenye pembe kubwa inayozidi digrii 70. Hata hivyo, tofauti kubwa na mifumo mingine minne ni kwamba mingine hiyo ina gimba kubwa la ziada—kama vile sayari kubwa ya gesi au nyota nyingine—ambalo ndilo linaloaminika kusababisha mkengeuko huo mkubwa wa mzunguko, wakati GJ 3090 b yenyewe inaonekana kuwa pweke bila kuwa na msindikiza mkubwa wa aina hiyo.

Kutokuwepo kwa gimba hilo kubwa kumewapa changamoto wanasayansi na kuwafanya wagundue mambo mapya, ambapo mtafiti Vincent Bourrier wa UNIGE ameeleza kuwa hali hiyo inawasukuma kuchunguza nadharia na uwezekano mwingine wa kisayansi, ikiwemo uwezekano kwamba nyota hiyo ya GJ 3090 ilimeza na kuunganisha diski ya pili ya nyuma iliyokuwa na mwelekeo wa kinyume wakati mfumo huo ulikuwa unaundwa tangu awali.

Wakati huo huo, wataalamu hao wa anga za juu wanajadili pia uwezekano mwingine kupitia maoni ya kitaalamu kwamba sayari hiyo labda iliwahi kuwa gimba huru lililonaswa kutoka mfumo mwingine wa mbali au ilisukumwa kwenye mzunguko huo na mgongano mkubwa wa kikosmiki huko nyuma kabla ya nyota hiyo kubakia yenyewe.

Utafiti huu wa kina na matokeo yake rasmi unafungua ukurasa mpya wa uelewa kuhusu namna mifumo ya sayari inavyoweza kuundwa na kubadilika katika ulimwengu wetu mpana.

Post a Comment

Previous Post Next Post