" WARIOBA AHUBIRI UMOJA BADALA YA KULIGAWA TAIFA - MALOTO

WARIOBA AHUBIRI UMOJA BADALA YA KULIGAWA TAIFA - MALOTO




Mwandishi wa makala za siasa, Luqman Maloto, amesema Tanzania inahitaji wakosoaji, lakini pia inahitaji viongozi wastaafu wenye hadhi ya 'Statesman' ambao wanaweza kuwa washauri na wapatanishi katika nyakati za misukosuko ya kisiasa, akibainisha kuwa mkosoaji anayejenga uadui na uongozi uliopo madarakani hupoteza nafasi ya kuaminika kama mshauri wa Nchi.


Maloto amesema Jaji Joseph Warioba, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu na Waziri Mkuu mstaafu, ana uzoefu mkubwa wa kiuongozi unaompa hadhi ya kuwa 'Statesman' na mshauri wa viongozi waliopo madarakani. Hata hivyo, amesema Warioba amejipambanua zaidi kama mkosoaji kuliko mshauri na mpatanishi, hali ambayo kwa maoni yake inaweza kupunguza uwezo wake wa kuaminika na pande zote katika kutafuta suluhu za changamoto zinazolikabili taifa.


Amesema mshauri hawezi kuwa mtu ambaye kila mara anaonekana akimshambulia hadharani mtu anayepaswa kumshauri, akieleza kuwa hali hiyo humfanya mshauriwa kumuona kama mpinzani badala ya mshauri, akitolea mfano kauli ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyowahi kusema kwamba angeshangaa kama Warioba na wenzake wangempongeza, akisema kauli hiyo inaonesha namna mtu anavyoweza kutambulika katika nafasi ya mkosoaji na hivyo kupoteza nafasi ya kuonekana kama mshauri.


Maloto amehoji pia kwa nini Warioba hajawahi kujitokeza hadharani kupongeza hatua chanya za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, akitolea mfano kukamilika na kuzinduliwa kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), akibainisha kuwa kwa hadhi yake hakupaswa kuwa na upande bali anatakiwa kuwa sehemu ya suluhu, akitumia uzoefu wake kuunganisha pande zinazokinzana na kuhakikisha masilahi ya taifa yanawekwa mbele.


Akizungumzia matukio ya Oktoba 29, 2025, Maloto amesema Tanzania inahitaji watu wenye hadhi ya 'Statesman' kutumia ushawishi wao kuponya taifa na kuhamasisha mazungumzo na maridhiano, akimkosoa kwa kauli yake kwamba idadi ya vifo vilivyotokana na matukio hayo ilikuwa kubwa kuliko vifo vya Vita ya Kagera, taarifa ambazo ni za mtandaoni na si hesabu rasmi, hivyo hazikupaswa kutumiwa na mtu mwenye hadhi yake.


Kwa ujumla, Maloto amesema Warioba anapaswa kujiuliza kama kuendelea kuikosoa Serikali hadharani kutasaidia kumaliza mivutano ya kisiasa nchini, akisisitiza kuwa historia ya Tanzania inaonesha mazungumzo na maridhiano kuwa miongoni mwa njia zilizosaidia taifa kuvuka vipindi vigumu. Amesema lengo la Statesman linapaswa kuwa kuhakikisha Tanzania inashinda, badala ya upande mmoja wa kisiasa kushinda, na kwamba kwa kujipambanua kama mkosoaji, Warioba amepoteza kwa kiasi kikubwa hadhi ya kuonekana kama mshauri na mpatanishi wa Rais.

Post a Comment

Previous Post Next Post