" AKAMATWA KWA KUTOA TAARIFA YA UONGO KUWA AMETEKWA

AKAMATWA KWA KUTOA TAARIFA YA UONGO KUWA AMETEKWA


Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limemkamata mwanamke mmoja aitwaye Vivian Jackson Salekwa mkazi wa Majengo Jijini Arusha kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa kama ambavyo ilichapishwa katika mtandao ya kijamii na mtu aitwaye Twaha Mwaipaya.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani humo, SACP Justine Masejo amebainisha kuwa taarifa ya kupotea kwa mtu huyo iliripotiwa Oktoba 10, 2026, na kueleza kuwa mtuhumiwa huyo akiwa njiani maeneo ya Majengo, watu wasiojulikana wakiwa na gari nyeusi walimchukua na kuondoka naye kusikojulikana.

Kamanda Masejo amesema mara baada ya kupokea taarifa hiyo, walianza uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo, ambapo Oktoba 16, 2026 walibaini kuwa, Mhanga Vivian hakuwa ametekwa wala kuchukuliwa na watu bali alifanya hivyo ili kuficha tukio la kutishia kuua linalomkabili Mpenzi wake aitwaye Castus Bagambisa, linaloendelea kuchunguzwa huko Mkoani Kilimanjaro.

Ameendelea kufafanua kuwa uchunguzi huo umebaini kuwa, mtuhumiwa huyo alimtuma binti wake wa kazi aitwaye Mariam Mwinjuma ili kusudi afikishe taarifa hizo za uongo kwa wazazi wake kuwa ametekwa na kwenda kujificha.

Aidha, Jeshi hilo tunawashikilia watu watatu ambao ni Vivian Jackson Salekwa, Mariam Mwinjuma na Castus Bagambisa kuhusiana na tukio hilo kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.

Jeshi la Polisi mkoani humo limeonya baadhi ya watu wenye tabia za kutoa na kusambaza taarifa za uongo zinazoleta taharuki katika jamii, kwani wanapaswa kutambua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, na yeyote atakayebainika atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huo huo, Jeshi hilo limesema linaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la mtu mmoja mwanamke kukutwa akiwa amefariki dunia muda wa usiku huko katika nyumba ya kulala wageni iliyopo maeneo ya Kaloleni Jijini Arusha.

Katika taarifa hiyo, limetoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, na limeomba mtu yoyote mwenye taarifa zinazohusiana na tukio hili azifikishe katika kituo chochote cha Polisi.

Post a Comment

Previous Post Next Post