
Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeonya kuwa halitasita kufuta matokeo ya mtahiniwa yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu katika Mtihani wa Kidato cha Nne wa mwaka 2026, unaotarajiwa kuanza Oktoba 19 hadi Novemba 6 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Octoba 18,2026 Katibu Mtendaji wa NECTA Profesa Said Ally Mohammed amesema maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika, yakiwamo usambazaji wa karatasi za mitihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka nyingine muhimu katika halmashauri na manispaa zote za Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimekamilisha maandalizi ya vituo, kutoa mafunzo kwa wasimamizi na kuweka mikakati ya kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu, huku usalama wa vituo ukiimarishwa ili kuhakikisha mtihani unafanyika kwa utulivu.
Amesisitiza kuwa wasimamizi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa umakini, uadilifu na weledi, kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya mitihani, ili kuhakikisha kila mtahiniwa anapata haki yake na kufanya mtihani ndani ya muda uliopangwa.
Kwa mujibu wa NECTA, watahiniwa wenye mahitaji maalum wanapaswa kupatiwa mazingira yanayowawezesha kufanya mtihani kwa usawa, yakiwamo maandishi ya nukta nundu kwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu.
Aidha, watahiniwa hao wanapaswa kuongezewa muda wa dakika 20 kwa kila saa katika somo la Hisabati ya Msingi na dakika 10 kwa kila saa katika masomo mengine, kwa mujibu wa mwongozo wa Baraza hilo.
Baraza limewataka wamiliki wa shule kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wakati wa mtihani, huku wakuu wa shule wakitakiwa kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na NECTA na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mitihani.
Aidha baraza limeonya kuwa halitasita kufuta kituo chochote cha mtihani endapo litathibitisha kuwepo kwa matukio au vitendo vinavyohatarisha usalama wa mtihani. Hatua hiyo inalenga kulinda uadilifu wa mchakato wa mitihani na kuhakikisha matokeo yanayotolewa yanaakisi uwezo halisi wa watahiniwa.
NECTA pia imezitaka jamii na wananchi kuhakikisha watu wasiohusika hawaingii katika maeneo ya shule yanayotumika kama vituo vya mitihani katika kipindi chote cha mtihani, ili kuwawezesha watahiniwa kufanya mitihani yao katika mazingira ya amani na utulivu.
Ameongeza kuwa Mtihani wa Kidato cha Nne una umuhimu mkubwa kwa kuwa hupima umahiri wa wanafunzi katika masomo waliyosoma kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne. Matokeo yake pia hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano na kozi mbalimbali za kitaaluma, zikiwamo afya, kilimo na ufundi.
Jumla ya watahiniwa 667,040 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo ambapo kati ya 664,085 ni watahiniwa wa shule na 22955 ni watahiniwa wa kujitegemea huku wavulana wakiwa ni 297,309 sawa na asilimia 46.16 na wasichana 297,776 sawa na asilimia 53.84 aidha wapo watahiniwa wa shule 910 ni wenye uhitaji maalum.
Katika hatua nyingine, NECTA imewataka wananchi wanaobaini vitendo vya udanganyifu kutoa taarifa kupitia namba ya simu 0759360000 au barua pepe esnecta@necta.go.tz, ikiahidi kufanyia kazi taarifa hizo na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Post a Comment