" Dkt. Mwinyi Atoa Rai Nzito Kuhusu Ulinzi wa Wafanyakazi Wahamiaji kwenye Mkutano wa Pili wa Doha

Dkt. Mwinyi Atoa Rai Nzito Kuhusu Ulinzi wa Wafanyakazi Wahamiaji kwenye Mkutano wa Pili wa Doha




Na Beda Msimbe, BSKY Media

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa pamoja na fursa kubwa za ajira zinazopatikana katika mataifa ya Ghuba, wafanyakazi kutoka bara la Afrika bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali nzito zinazohitaji dharura ya ushirikiano wa dhati na uwajibikaji wa pamoja kati ya nchi za Afrika na ukanda wa GCC+.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 6, 2026, akiwa mgeni rasmi aliyemwakilishi Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Majadiliano ya Pili ya Doha (Doha Dialogue II), Dkt. Mwinyi alitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mifumo ya uajiri isiyo ya haki, gharama kubwa za uajiri, kunyimwa taarifa muhimu kabla ya safari, kutolipwa au kucheleweshewa mishahara, mazingira yasiyo salama ya kazi, upatikanaji mdogo wa haki, na mapungufu makubwa katika mifumo ya ulinzi wa kijamii.

Dkt. Mwinyi alifafanua kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, ulinzi wa haki za mfanyakazi anayekwenda kufanya kazi katika nchi za Ghuba unapaswa kuanza kabla hajatoa hatua ya kuondoka nchini mwake, kwa kuhakikisha anapatiwa taarifa sahihi na za kina kuhusu mkataba wa ajira, stahiki zake, mishahara, na mazingira halisi ya kazi anayokwenda kukutana nayo.

Alisisitiza kuwa mchakato wa uajiri lazima uwe wa wazi, unaoweza kuthibitishwa na kuzingatia viwango vinavyokubalika kimataifa, huku akitaka majadiliano hayo yaelekeze nguvu kubwa katika utekelezaji wa sera badala ya kubaki kwenye ahadi na matamko matupu.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na nchi za Ghuba( GCC+) kwa kuzingatia misingi ya manufaa ya pamoja na uwajibikaji wa pamoja.

Kwa upande wake, Kamishna wa Afya, Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Balozi Amma Adoma Twum-Amoah, alieleza kuwa kasi ya utekelezaji wa ahadi zilizowekwa katika mijadala ya nyuma imekuwa ya polepole, akapendekeza kuundwa kwa utaratibu wa kiufundi wa pamoja utakaosimamia utekelezaji wa maamuzi ili kuleta matokeo chanya yanayopimika kwa wafanyakazi wahamiaji.
















Naye Mkurugenzi wa Kanda wa Nchi za Kiarabu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Dkt. Ruba Jaradat, alibainisha kuwa ushirikiano kati ya ILO, serikali, na wadau wa kazi katika nchi za Ghuba umeanza kuzaa matunda ya kivitendo, akitoa mifano ya nchi kama Saudi Arabia ambako marekebisho ya sheria za kazi yamefanyika ili kuongeza ulinzi kwa wafanyakazi, Ufalme wa Kiarabu (UAE) unaotekeleza programu za kuboresha rasilimali watu, na Oman iliyopiga hatua kubwa katika ulinzi wa kijamii.

Wakati huo huo, Serikali ya Tanzania imebainisha kuwa uhamaji wa nguvu kazi umegeuka kuwa nguzo kuu ya uchumi wa kisasa, ambapo kupitia juhudi za makusudi za kupanua ushirikiano wa kimataifa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, jumla ya Watanzania 15,241 wamefanikiwa kupata ajira rasmi na zilizothibitishwa katika nchi za Ghuba kuanzia mwaka 2022 hadi Agosti 2026.

Akizungumza katika mkutano huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu alisema ili kulinda nguvu kazi hiyo, Serikali imeimarisha mifumo ya kisheria ikiwemo udhibiti wa Wakala Binafsi za Ajira, kusaini mikataba ya nchi mbili, kuzindua Mkopo wa Ughaibuni kupitia Benki ya CRDB na TRAA ili kusaidia gharama za safari, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kikoni kufuatia kukabidhiwa uenyekiti wa RMFM mnamo Agosti 2026.



Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Kazi wa Qatar, Mhe. Dkt. Ali bin Samikh Almarri;; Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana na Uwezeshaji Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir Mrembo; Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Awesi Mohamed, pamoja na Taasisi mbalimbali za kimataifa, wajumbe kutoka nchi zaidi ya 33, zikiwemo nchi za Afrika, Nchi Wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC+), Jordan na Lebanon.

Post a Comment

Previous Post Next Post