Mbunge wa Rombo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza kuahirishwa kwa Rombo Marathon na Ndafu Festival zilizokuwa zifanyike Disemba 23, 2026 katika Misitu ya Rungai, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.
Prof. Mkenda amesema uamuzi huo umechukuliwa kutokana na tahadhari za uwepo wa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya hewa ya El Niño, akieleza kuwa si busara kuendelea kuwaalika washiriki kutoka maeneo mbalimbali kutumia fedha zao kushiriki katika shughuli hiyo wakati kuna uwezekano wa kutokea madhara yanayoweza kuhatarisha usalama wao.
Akizungumza jijini Dodoma Oktoba 17, 2026 Prof. Mkenda amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya mashauriano na bodi ya maandalizi ya matukio hayo, huku akisisitiza kuwa tahadhari na usalama wa washiriki ni jambo la msingi kuliko kuendelea na tukio hilo kwa sababu ya umaarufu wake. Ameongeza kuwa maandalizi yataendelea kwa ajili ya kuhakikisha Rombo Marathon na Ndafu Festival za mwaka 2027 zinafanyika kwa ukubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, matukio hayo yamekuwa na manufaa mbalimbali, ikiwemo kutoa burudani kwa washiriki na familia zao, pamoja na kukuza utalii wa ndani kupitia mandhari ya Misitu ya Rungai na maeneo ya Mlima Kilimanjaro.
"Washiriki wamekuwa wakifika kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi, huku baadhi ya viongozi na wanasiasa kutoka nchi jirani wakishiriki katika mbio hizo, ameongeza Prof. Mkenda
Aidha, Prof. Mkenda amesema Rombo Marathon imekuwa ikichangia maendeleo ya jamii kupitia fedha zinazopatikana, ambazo zimeelekezwa katika kuboresha shule na huduma za afya, ikiwemo Hospitali ya Huruma. Ameeleza kuwa Ndafu Festival pia imekuwa ikitumika kama sehemu ya kuvutia wageni na kuendeleza utalii na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.
Akizungumzia uamuzi wa kuahirisha tukio hilo, Prof. Mkenda amesema licha ya kusikitishwa na uamuzi huo, ni muhimu kwa waandaaji kuwajibika kwa washiriki kwa kuzingatia tahadhari za wataalamu kuhusu hali ya hewa na kwamba uamuzi huo unalenga kuhakikisha usalama wa watu, huku akiwataka wadau kuendelea kujiandaa kwa ajili ya Rombo Marathon na Ndafu Festival mwaka 2027.
Post a Comment