" MASHINDANO YA MOOT COURT 2026 KUFUNGUA FURSA KWA WANASHERIA VIJANA

MASHINDANO YA MOOT COURT 2026 KUFUNGUA FURSA KWA WANASHERIA VIJANA

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa TRA Paul Walalaze, ameeleza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikishirikiana VIctor's Hub Limited waandaaji wa mashindano (Moot Court Competition) tangu hatua za awali, ikiwemo kutoa ufadhili ili kufanikisha shughuli hiyo.

Walalaze, amesema mashindano hayo yana umuhimu mkubwa katika kuwaandaa wanafunzi wa sheria kuwa wataalamu watakaokuja kutoa ushauri kwa walipa kodi na wawekezaji, hivyo kusaidia kuongeza uelewa wa sheria za kodi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Ameongeza kuwa uwekezaji nchini Tanzania unahusisha wawekezaji wa ndani na wa nje, hivyo ni muhimu kwa wataalamu wa sheria kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mifumo ya kodi na sheria zinazohusiana na uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Victor’s Hub Limited, Edith Michael Mtweve, amesema mashindano hayo yamefanyika kwa mwaka wa sita mfululizo, yakilenga kuwajengea wanafunzi wa sheria ujuzi wa kitaaluma na kuwawezesha kuwa wanasheria mahiri ndani na nje ya nchi.

Amesema katika kuandaa mashindano hayo, wamefikia wanafunzi wa vyuo mbalimbali katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa na Mbeya, huku wakiendelea na juhudi za kuwafikia wanafunzi wengine nchini.

Mtweve, amesema mada ya mwaka huu inahusu utozaji kodi katika uwekezaji, ikiwapa wanafunzi fursa ya kujifunza namna sheria za kodi na sheria za kimataifa zinavyotumika katika masuala ya uwekezaji na namna ya kujenga hoja za kisheria mbele ya majaji.

Naye mwanafunzi wa mwaka wa pili wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Roslin Sami, amesema amefurahi kuchaguliwa kushiriki katika hatua ya mwisho ya mashindano hayo, akieleza kuwa ni fursa ya kuonesha uwezo wake wa kujenga hoja na kutumia maarifa ya sheria.

Kwa upande wake, Jimmyson Mabati, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Katoliki Mwenge kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro, amesema mashindano hayo yanawasaidia wanafunzi kuelewa kwa kina sheria za kodi, vivutio vya uwekezaji na namna sera na sheria zinavyoweza kusaidia kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post