" ELIMU YA HOMA YA INI YATOLEWA KASULU MJI, WATUMISHI NA WANANCHI WASISITIZWA KUPIMA NA KUPATA CHANJO.

ELIMU YA HOMA YA INI YATOLEWA KASULU MJI, WATUMISHI NA WANANCHI WASISITIZWA KUPIMA NA KUPATA CHANJO.


Halmashauri ya Mji Kasulu imeendelea kuimarisha uelewa wa watumishi wa Umma kuhusu kinga, upimaji na tiba ya Homa ya Ini aina ya Hepatitis B kwa lengo la kuwahamasisha kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo pamoja na madhara yake.Elimu hiyo imetolewa kupitia mafunzo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri katika ukumbi wa Fatina H. Laay, ambapo watumishi wamejengewa uelewa kuhusu njia za maambukizi ya virusi vya Hepatitis B, umuhimu wa kupima afya mapema na matumizi ya chanjo kama njia muhimu ya kujikinga na ugonjwa huo.Katika mafunzo hayo, watumishi wamehimizwa kuepuka kuchangia vifaa vyenye ncha kali, ikiwemo sindano na nyembe, pamoja na kuzingatia tahadhari za kujikinga na maambukizi kupitia damu. Aidha, wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.Hepatitis B ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoathiri ini na unaweza kusababisha madhara makubwa, yakiwemo ugonjwa wa ini ujulikanao kama cirrhosis na saratani ya ini, iwapo maambukizi ya muda mrefu hayatagunduliwa na kufuatiliwa ipasavyo.Vilevile katika mafunzo hayo, imesisitizwa umuhimu wa kuepuka unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Hepatitis B badala yake jamii imetakiwa kuwapa ushirikiano na kuwahimiza kupata huduma za afya huku ikikumbushwa kuwa ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa chanjo.Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia J. Simbeye amewahimiza watumishi na wananchi kwa ujumla kuzingatia elimu ya afya wanayoipata, kupima afya zao na kutumia huduma zinazotolewa katika vituo vya afya ili kubaini maambukizi mapema na kupata ushauri pamoja na huduma stahiki.Halmashauri ya Mji Kasulu inaendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Ini ili kujikinga na maambukizi na madhara yake.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post