Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, ametoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Mwalukwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, akiwataka kudumisha amani, kusalimisha silaha haramu na kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazotarajiwa kunyesha siku za hivi karibuni.
Akizungumza na wananchi hao kupitia kampeni ya “Ongea na Kamanda”, SACP Magomi amesisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na utulivu, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuzuia uhalifu na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.
Katika mkutano huo, Kamanda Magomi ametoa elimu kuhusu kampeni ya usalimishaji wa silaha haramu, akiwataka wananchi wanaomiliki silaha bila vibali halali kuzisalimisha katika ofisi za serikali za vijiji na mitaa, ofisi za watendaji wa kata pamoja na vituo vya polisi.
Aidha, amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhama na kwenda maeneo salama kutokana na mvua zinazotarajiwa kunyesha siku za hivi karibuni, kwa kuzingatia tahadhari zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Akizungumzia suala la ulinzi wa mtoto, SACP Magomi amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na mazingira salama ya kujifunzia. Pia, amewahimiza wanafunzi waliohudhuria mkutano huo kusoma kwa bidii na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwafanya wakatishe masomo yao kabla ya kufikia malengo yao.
Katika kipindi cha maswali na majibu, wananchi walihoji uhalali wa Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa bila kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji. Akijibu hoja hiyo, Kamanda Magomi alieleza kuwa utaratibu wa kumkamata mtuhumiwa hutegemea mazingira na aina ya mtuhumiwa, akibainisha kuwa kutoa taarifa mapema katika kila tukio kunaweza kumpa mtuhumiwa nafasi ya kutoroka na hivyo kuathiri utekelezaji wa majukumu ya polisi.
Kwa upande wao, wananchi walilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kutoa elimu na kuwapa fursa ya kuwasilisha maoni yao kupitia kampeni hiyo. Hata hivyo, walieleza changamoto mbalimbali, ikiwemo mgogoro wa ardhi, ambao haukuwa suala la moja kwa moja la kiusalama.
Kufuatia hali hiyo, changamoto zilizowasilishwa zilipokelewa kwa ajili ya kuwasilishwa kwa mamlaka na wahusika wanaohusika ili ziweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Kampeni ya “Ongea na Kamanda” ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kuimarisha mawasiliano na wananchi, kutoa elimu ya usalama na kupokea kero zinazohitaji ufumbuzi kwa kushirikiana na jamii pamoja na mamlaka nyingine husika.
PROFESSOR MGOKO EPISODE 06🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment