Na, Egidia Vedasto,Misalaba Media, Arusha.
Waziri wa Ujenzi Masanja Kadogosa wakati akikagua mradi wa Ujenzi wa barabara Jijini Arusha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuleta maendeleo nchini, akisema wananchi wa Arusha wanaona na kuthamini kazi inayofanyika chini ya uongozi wake, hususan katika kuboresha miundombinu ya barabara.
Amesema ujenzi wa barabara unaoendelea mkoani Arusha haupaswi kuonekana kama maandalizi ya AFCON pekee, bali ni uwekezaji wa muda mrefu ambao utaendelea kuwa na manufaa kwa wananchi hata baada ya mashindano hayo kumalizika. Amesema barabara hizo zitasaidia kufungua zaidi Jiji la Arusha na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa barabara mbalimbali, ikiwemo kipande cha kilomita 7.4 kutoka Mbauda hadi Arusha Bypass pamoja na barabara nyingine zinazolenga kuunganisha maeneo mbalimbali ya Arusha. Amesema lengo kubwa ni kuhakikisha Arusha inakuwa na miundombinu bora inayolingana na nafasi yake katika shughuli za kitaifa na kimataifa.
"Maandalizi ya AFCON yanahitaji ushirikiano wa Serikali nzima, si Wizara moja pekee, wizara na taasisi mbalimbali zinapaswa kushirikiana kuhakikisha kazi zinazohusiana na ujenzi wa miundombinu na maandalizi ya mashindano hayo zinakamilika kwa wakati".
Akizungumzia nafasi ya Arusha katika matukio ya kimataifa, amesema Jiji hilo limeendelea kuwa mwenyeji wa mikutano mikubwa, ikiwemo mikutano ya kimataifa ya Bunge, jambo analosema ni ushahidi wa nafasi ya Tanzania katika masuala ya utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria. Amesema uwepo wa wabunge na viongozi kutoka nchi mbalimbali katika mikutano hiyo ni ishara ya imani waliyonayo kwa Tanzania.
Amesema"Uongozi haupimwi kwa maneno pekee bali kwa matendo na namna wananchi na watu wengine wanavyouona utendaji wa viongozi. Amesema viongozi wanapaswa kujiuliza namna wanavyoonekana kwa watu wanaowaongoza na kuhakikisha matendo yao yanajenga taswira nzuri ya nchi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Eng.Reginald Masawe amesema utekelezaji wa mradi wa barabara unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, hususan kwenye njia zinazounganisha katikati ya jiji na maeneo ya nje.
Amesema kwa ujumla mradi huo unahusisha ujenzi wa takribani kilomita 70 kwa gharama ya shilingi bilioni 260, huku Serikali ikiwa tayari imelipa shilingi bilioni 21 kama malipo ya awali ili kuwezesha utekelezaji wa mradi kuanza na kuendelea kwa kasi.
Ameeleza "Mkandarasi anaendelea na kazi usiku na mchana, ikiwemo kwenye kipande cha kilomita 13 kinachohusishwa na maandalizi ya AFCON, kwa lengo la kuhakikisha kinamalizika kwa wakati, sehemu nyingine za mradi huo zitaendelea kutekelezwa kwa muda wa takribani miaka mitano hadi kukamilisha kilomita zote 70".
Aidha, Eng.Masawe amesema kwa sasa msongamano wa magari katika kipande hicho cha kilomita 13 umefikia kiwango cha takribani magari 846, hali inayodhihirisha umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo, huku maeneo mengine ya mradi yakiendelea kufanyiwa kazi na mkandarasi.
Amesema "Mradi huo unasimamiwa na kitengo cha ndani cha TANROADS kinachojulikana kama TANROADS Engineering Consulting Unit, na utekelezaji wake unaendelea vizuri, barabara hiyo inaanzia Chuo cha Ufundi Arusha na kuendelea hadi eneo la roundabout inapokutana na Kisongo Bypass, huku kutoka eneo hilo kuelekea Matevesi na uwanja wa ndege kukiwa na kipande cha takribani kilomita 1.8 kinachohitaji ujenzi kwa kiwango kinachofaa kutokana na umuhimu wake katika mtandao wa barabara"
Eng. Masawe ameeleza kuwa eneo hilo linahitaji pia kushughulikiwa suala la fidia, huku hatua za usanifu na tathmini zikihitaji kukamilishwa ili kupata gharama halisi za utekelezaji na kuwezesha Serikali kupanga hatua zinazofuata.
Vile vile Waziri wa habari, utamaduni Sanaa na michezo na Mbunge wa jimbo la Arusha Paul Makonda amesema mafanikio yanayoonekana katika ujenzi wa miundombinu Arusha yanatokana na uwezo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza kazi bila makelele, akisema wananchi wameona matokeo ya kazi hiyo na ndiyo maana wanaendelea kumuunga mkono na kumuombea.
Amemshukuru Waziri na Wizara ya ujenzi kwa ushirikiano wanaoutoa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akimtaja mtangulizi wake, Abdallah Ulega pamoja na wataalamu wa wizara, Katibu Mkuu na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, kwa namna walivyoshirikiana na viongozi wa Arusha kuhakikisha miradi inatekelezwa.
Makonda amesema matarajio yake ni kuona kwa kasi mpya ya uongozi wa Waziri, Arusha inakamilisha miradi iliyopo na wananchi wanaanza kutumia barabara za lami kama walivyoahidiwa. Amesema siasa ina maana pale ahadi zinazotolewa kwa wananchi zinapotekelezwa na kuleta mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha yao.
Amesema "Kwa muda mrefu Arusha iliachwa nyuma katika baadhi ya miradi ya barabara, hali iliyowafanya wananchi kutumia barabara zenye changamoto kubwa. Hata hivyo, amesema utekelezaji wa miradi ya sasa umeanza kubadilisha hali hiyo na kuwaondoa wananchi katika historia ya kusikia ahadi za ujenzi na kuwawezesha kuona barabara za lami zikijengwa"
Makonda ameiomba Serikali kuangalia kipande cha barabara kinachohitaji fidia chenye urefu wa takribani kilomita nne ili kukamilisha muunganiko wa barabara za njia nne kutoka Arusha Bypass hadi barabara zinazotoka Kisongo kuelekea Kilombero. Amesema kukamilika kwa kipande hicho kutarahisisha usafiri na kuunganisha maeneo muhimu ya jiji.
Amesema wananchi hawataki tena kuona barabara mpya zikianza kutumika na muda mfupi baadaye kuanza kuwa na mashimo, bali wanataka miundombinu itakayodumu kwa miaka 20 hadi 30 na kuwa sehemu ya historia watakayowaachia vizazi vijavyo.
Charles Mushi dereva wa magari ya utalii ameipongeza serikali ya awamu ya sita na kusema kuwa "hii ndio Arusha tuliyoisubiri Kwa muda mrefu, nitajivunia sana kazi yangu ya kuwaongoza Watalii katika barabara safi za lami zisizo na mashimo"
Post a Comment