JUKWAA HURU LA WAHARIRI TANZANIA (JUWATA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JUWATA YAMPONGEZA ZUNGU KUWA RAIS WA MKUTANO WA 153 WA IPU
Uongozi wa Jukwaa Huru la Wahariri Tanzania (JUWATA) unampongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
Mhe. Zungu amechaguliwa leo, Jumanne, Oktoba 6, 2026, baada ya jina lake kupendekezwa na Spika wa Bunge la Uingereza (House of Commons), Sir Lindsay Hoyle, wakati wa Mkutano wa Baraza la Uongozi la IPU.
Hatua hiyo pia imeungwa mkono na Spika kutoka Falme za Kiarabu pamoja na Bunge la Uganda, hatua inayoendelea kuipa Tanzania heshima na nafasi kubwa katika diplomasia ya mabunge duniani.
JUWATA inaamini kuwa kuchaguliwa kwa Mhe. Zungu kushika wadhifa huo ni heshima kubwa kwa Tanzania na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba atatumia nafasi hiyo kuongoza kwa weledi, hekima na busara, huku akisimamia misingi ya ushirikiano, amani, demokrasia na diplomasia ya mabunge.
Aidha, JUWATA inampongeza Mhe. Zungu kwa uongozi wake wa Bunge la Tanzania, ambao kwa hatua hii umeendelea kuliletea Taifa heshima na kutambulika katika medani ya kimataifa.
TANZANIA YAWEKA HISTORIA IPU
JUWATA Pia inatambua kauli ya Mhe. Zungu kwamba Tanzania imeweka historia katika Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU, kwa kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya IPU, iliyoanzishwa mwaka 1889, viongozi wawili kutoka Tanzania wanashika nafasi za juu katika mkutano huo.
Mhe. Zungu sasa ni Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU, wakati Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ni Rais wa IPU.
Kwa mujibu wa Mhe. Zungu, hali hiyo ni historia kubwa kwa Tanzania na itaendelea kubaki katika kumbukumbu za Taifa.
JUWATA inaamini kuwa mafanikio hayo yanaakisi nafasi inayozidi kukua ya Tanzania katika diplomasia ya kimataifa na katika kujenga ushirikiano kati ya mabunge ya nchi mbalimbali duniani.
JUWATA YAPONGEZA DIPLOMASIA YA TANZANIA
JUWATA pia inapongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuiwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU.
Kwa mujibu wa Mhe. Zungu, ushiriki wa Spika wa Bunge la Uingereza, Sir Lindsay Hoyle, katika Mkutano wa 153 wa IPU unaofanyika Arusha ni tukio la kihistoria, kutokana na kutohudhuria kwake kikao kamili cha IPU kwa zaidi ya miaka 40.
JUWATA inaona tukio hilo kuwa sehemu ya mafanikio ya diplomasia ya Tanzania na fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mabunge ya mataifa mbalimbali duniani.
JUWATA YAMUUNGA MKONO ZUNGU
JUWATA inamtakia Mhe. Mussa Azzan Zungu kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake mapya kama Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU na inaamini kuwa atatumia nafasi hiyo kuendelea kuijengea Tanzania heshima, kuimarisha diplomasia ya mabunge na kukuza masuala ya amani, demokrasia na maendeleo duniani.
Kwa niaba ya JUWATA, tunampongeza kwa dhati Mhe. Zungu pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua hii kubwa ya kihistoria.
Mungu ibariki Tanzania.
Richard Mwaikenda
Mwenyekiti – JUWATA
6 Oktoba 2026
PROFESSOR MGOKO EPISODE 04
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment