Na Silivia Amandius, Kagera.
Mkoa wa Kagera unatarajia kusajili kaya 38,217 zenye jumla ya watu 84,934 katika awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi, wakiwemo kaya zenye uhitaji, makundi maalumu, vikundi vya ushirika na jamii kwa ujumla.
Akizindua awamu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, alisema kaya maskini zinazotambuliwa rasmi zitasajiliwa bila kuchangia fedha, huku kaya nyingine, vikundi na vyama vya ushirika vikichangia Shilingi 150,000 kwa mwaka, kiasi kitakachowezesha watu sita kupata huduma za matibabu kupitia vifurushi vya mpango huo.
Kanali Kido aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha usajili na utambuzi wa wanufaika unafanyika hadi katika ngazi za vijiji na mitaa. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi, watendaji na wadau ni muhimu katika kuwafikia wananchi wanaostahili na kuwapatia taarifa sahihi kuhusu mpango huo.
Kwa upande wake, Meneja wa NHIF mkoani Kagera, Ismail Kangeta, alisema katika awamu ya kwanza jumla ya kaya 15,284 zenye wakazi 67,451 zilisajiliwa, sawa na asilimia 76 ya lengo la asilimia 80 lililokuwa limewekwa. Alieleza kuwa mfuko huo uko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuongeza mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya na kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi.
Mpango huo unalenga kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi na kuwawezesha kupata huduma za afya wanapozihitaji. Kaulimbiu ya mpango huo ni “Bima ya Afya kwa Wote kwa Uhakika wa Matibabu.”
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment