" RC MHITA AZINDUA AWAMU YA PILI YA BIMA YA AFYA KWA WOTE SHINYANGA

RC MHITA AZINDUA AWAMU YA PILI YA BIMA YA AFYA KWA WOTE SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amezindua awamu ya pili ya kampeni ya usajili wa Bima ya Afya kwa Wote, iliyoambatana na huduma za upimaji wa afya bila malipo na elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhita amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma hizo kwa kujiunga na bima ya afya, akieleza kuwa hatua hiyo itawasaidia kupunguza gharama za matibabu ambazo wamekuwa wakizitumia wanapokabiliwa na changamoto za kiafya.

Amesema afya bora ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla, hususan katika Mkoa wa Shinyanga ambao wananchi wake wengi wanajishughulisha na kilimo na uchimbaji wa madini, shughuli zinazohitaji nguvu na afya njema ili kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao.

Aidha, amewaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri na waratibu wa kampeni hiyo kusimamia utekelezaji wake kwa weledi na kuhakikisha wananchi wanapata elimu sahihi kuhusu bima ya afya, pamoja na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa katika maeneo yao.

Mhita ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira yanayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kuhusu utekelezaji wa kampeni hiyo, awamu ya kwanza ililenga kufikia kaya 14,325, ambapo kaya 11,285 zilifikiwa, sawa na asilimia 78.7 ya lengo lililokuwa limewekwa.

Awamu ya pili inalenga kufikia kaya 22,065 ambazo hazikuweza kufikiwa katika awamu ya kwanza, huku usajili wa makundi mbalimbali ya wananchi wanaohitaji bima ya afya ukiendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa kampeni hiyo.

Katika mpango huo, wananchi wanatarajiwa kufikiwa kupitia utaratibu wa usajili unaohusisha gharama ya Shilingi 150,000 kwa kila kaya yenye watu sita, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa wakati wa kampeni hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Shinyanga, Franklin Chekani, amesisitiza umuhimu wa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma za bima ya afya na taratibu za kujiunga, ili waweze kutumia huduma hizo kwa ufanisi na kupata matibabu wanapohitaji.

Naye Afisa Mipango Mkuu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Ahimidiwe Asseri, amewahimiza wananchi kuwasilisha malalamiko yao katika mamlaka hiyo pale wanapokutana na changamoto zinazohusiana na huduma za bima, ili ziweze kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Baadhi ya wananchi walionufaika na huduma za bima ya afya wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, wakieleza kuwa kuwa na bima kunawapa fursa ya kupata matibabu na kupunguza changamoto za gharama wanapougua.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akisalimiana na wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post