" MBIBO ASHIRIKI BONANZA LA MADINI, ASISITIZA MAZOEZI KWA AFYA NA UMOJA

MBIBO ASHIRIKI BONANZA LA MADINI, ASISITIZA MAZOEZI KWA AFYA NA UMOJA

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amewahimiza watumishi wa Wizara hiyo na taasisi zake kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya ya mwili na akili, kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kukuza umoja na mshikamano kazini.

Mbibo ametoa wito huo leo Septemba 17, 2026, aliposhiriki Bonanza la Madini lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari John Marline jijini Dodoma, akisisitiza kuwa mazoezi yanapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku badala ya kufanyika wakati wa matukio maalumu pekee.

Amesema michezo na mazoezi huchangia kujenga afya bora, kuimarisha mahusiano miongoni mwa watumishi na kuongeza ari na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, amewapongeza watumishi kwa kujitokeza kushiriki bonanza hilo na kuwataka kuendeleza mshikamano, umoja na utamaduni wa kufanya mazoezi kwa manufaa ya afya zao.

Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali, ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, kuvuta kamba, riadha, kukimbiza kuku, mbio za gunia na mbio za kubeba yai.

Washiriki walitoka Wizara ya Madini, Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Kituo cha Jiomolojia Tanzania (TGC). 

Post a Comment

Previous Post Next Post