Na WyEST,Tianjin, ChinaSerikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zimesaini hati ya makubaliano ya kuimarisha Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ufundi Stadi (TVET), kwa lengo la kuboresha ubora wa mafunzo, kuimarisha ushirikiano na viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Hati hiyo imesainiwa Oktoba 17, 2026, jijini Tianjin, na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb), kwa niaba ya Tanzania, na Naibu Waziri wa Elimu wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China China, Mhe. Wang Guangyan.
Makubaliano hayo yanatoa kipaumbele katika kuanzisha Karakana (Luban Workshop], kituo cha mafunzo ya ufundi kinachotumia teknolojia za kisasa pamoja na kuimarisha programu za uhandisi wa ujenzi, upimaji na uchoraji ramani, reli, barabara na madaraja. China pia imeahidi kutoa msaada wa kitaalamu kupitia mafunzo kwa walimu, uendelezaji wa mitaala ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ubadilishanaji wa wataalamu na matumizi ya mbinu za kisasa za ufundishaji.
Aidha, makampuni ya Kichina nchini Tanzania, hususan katika Sino–Tan Industrial Park na sekta za reli, nishati, madini na ujenzi, yamehimizwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, Serikali ya Tanzania itateua taasisi zitakazotekeleza makubaliano hayo na kuhakikisha programu zinaendana na Mfumo wa Kitaifa wa Sifa na Tuzo (TQF), ili kuimarisha ubora na uendelevu wa mafunzo.
Mbali na makubaliano hayo, Tanzania imenufaika na ushiriki wake katika Mkutano wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na nchi nyingine kuhusu uboreshaji wa mitaala, viwango vya mafunzo na uhusiano kati ya elimu na mahitaji ya soko la ajira.
Katika mkutano huo, Tanzania imeunga mkono Kiunzi cha Kimataifa cha Viwango vya Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi (Framework of World Vocational and Technical Education Standards), kinachotoa rejea ya hiari ya kulinganisha viwango huku kikiheshimu mifumo ya elimu ya kila nchi. Akizungumza kuhusu mfumo huo, Mhe. Ameir alisema unaendana na mageuzi ya elimu nchini yanayotekelezwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, linalolenga kujenga mfumo wa elimu unaozingatia ujuzi na umahiri.
Tanzania pia imependekeza vipaumbele vinne vya utekelezaji wa kiunzi hicho, ambavyo ni utambuzi wa pamoja wa sifa, upatikanaji wa ufadhili na vifaa vya kisasa, ubadilishanaji wa walimu na mafunzo, pamoja na tathmini ya hiari kwa ajili ya kujifunza kwa pamoja. Hatua hiyo inaipa nchi nafasi ya kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu viwango vya mafunzo na kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, ikiwemo na China.
Akizungumza katika kikao maalumu cha majadiliano Oktoba 16, 2026, Mhe. Ameir amesema elimu ya ufundi ni nyenzo muhimu ya kuunganisha nguvu kazi ya vijana wa Afrika na maendeleo endelevu ya kiuchumi. Alisisitiza umuhimu wa kuwaandaa vijana wenye ujuzi wa vitendo, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto katika sekta za reli, nishati, madini, kilimo, gesi na viwanda.
Ushiriki huo na makubaliano yaliyosainiwa yanatarajiwa kusaidia Tanzania kuboresha mafunzo ya ufundi, kuongeza uwezo wa wakufunzi na fursa za mafunzo kwa vitendo. Hatua hizo zinalenga kuandaa vijana wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, kuwawezesha kujiajiri na kuchochea ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Post a Comment