" WADAU WAMPONGEZA MWASISI WA TEHILAH FOUNDATION NA SHULE YA VANESSA KWA KULEA NA KUSOMESHA WATOTO YATIMA MKOANI MBEYA

WADAU WAMPONGEZA MWASISI WA TEHILAH FOUNDATION NA SHULE YA VANESSA KWA KULEA NA KUSOMESHA WATOTO YATIMA MKOANI MBEYA

​Na Lydia Lugakila,

Misalaba Media

Mbeya

​MWASISI wa Taasisi ya Tehilah Foundation pamoja na Shule ya Sekondari ya Vanessa, Bi. Shukran Gideon Mwasonjobe, amepongezwa na wadau mbalimbali kutokana na jitihada zake za kuwalea, kuwatunza na kuwajali watoto yatima pamoja na wale wanaotoka katika mazingira magumu, hatua iliyosaidia vijana wengi kupata elimu na fursa za ajira.

​Pongezi hizo zimetolewa na wadau mbalimbali wakati wa mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika katika eneo la shule hiyo iliyopo Isyesye, Mkoani Mbeya, ambapo walimwelezea Bi. Shukran kama mwanamke mwenye maono makubwa, moyo wa upendo na wa kipekee katika kubadilisha maisha ya watoto wenye uhitaji na kuwapatia matumaini ya baadaye.

​Akisoma risala katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Vanessa, Bw. Exon Mwakalikamo, alieleza kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafadhili kutoka Ujerumani, Australia na Switzerland. 

Wafadhili hao wanaongozwa na Mama Irmgard Hatum kutoka Ujerumani, ambaye amekuwa kiungo muhimu katika kusaidia kutimiza maono ya Mkurugenzi wa Tehilah Foundation.

​Bw. Mwakalikamo alieleza kuwa tangu mwaka 2006, zaidi ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ya 1,000 wamenufaika na ufadhili wa Tehilah Foundation kwa kushirikiana na wadau wa Ujerumani—wakiwemo marehemu Wolfgang, Irmgard, Nehemiah Getway, GMS, WMFF na Gerd ambapo wameweza kupata elimu kuanzia ngazi ya sekondari hadi chuo kikuu.

​Aidha, alibainisha kuwa wanafunzi hao wamelelewa vyema kitaaluma, kiroho na kinidhamu.

Amesema kuwa shule hiyo inachukua wanafunzi wa kike na wa kiume kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na ina malengo ya kuwa miongoni mwa shule bora nchini zenye kutoa elimu bora na kuzalisha wanafunzi wenye nidhamu na hofu ya Mungu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

​Katika kuendana na Sera ya Elimu nchini, Vanessa Sekondari imeanzisha Mafunzo ya Elimu Amali katika fani za ushoni na kompyuta na mafunzo haya yanatolewa kwa ufadhili wa Tehilah Foundation ikishirikiana na mashirika ya GMS na WMFF, yakiwa na lengo la kumwezesha mhitimu kuwa na ujuzi wa kujitegemea na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.

​Kuhusu mafanikio ya shule hiyo, Bw. Mwakalikamo alieleza kuwa shule imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, ambapo katika matokeo ya mtihani wa Taifa (NECTA) mwaka 2025 kwa kidato cha nne, wanafunzi wote walifaulu kwa kupata Daraja la Kwanza (Division I) na Daraja la Pili (Division II) pekee.

​Pia ameongeza kuwa shule hiyo imefanikiwa kujenga ukumbi wa kisasa pamoja na maabara ya fizikia kwa udhamini wa Tehilah Foundation ikishirikiana na mashirika ya GMS na WMFF kutoka Ujerumani ambapo maabara hiyo inatarajiwa kuongeza chachu, ufanisi na ufaulu katika masomo ya sayansi ili kuzalisha wataalamu wengi zaidi nchini.

​Mkuu wa shule huyo aliongeza kuwa wana matarajio makubwa juu ya wahitimu hao wa kidato cha nne mwaka 2026 ambapo watafanya vizuri sana katika mtihani wao wa Taifa unaotarajiwa kuanza Oktoba 19, 2026.

​Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika mahafali hayo, Bw. Kenedy Mwangapayo, alipongeza uongozi wa shule na Tehilah Foundation kwa maono makubwa na moyo wa kuwajali watoto yatima.

​Bw. Mwangapayo aliahidi kusaidia kulipa nusu ya gharama za masomo kwa wanafunzi wanaohitimu na kubahatika kuendelea na vidato vya juu shuleni hapo, pamoja na kutoa vifaa vya michezo vikiwemo mipira miwili na jezi ili kuboresha sekta ya michezo.

Hata hivyo aliwataka wahitimu hao kumtanguliza Mungu na kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao.

PROFESSOR MGOKO EPISODE 05

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment

Previous Post Next Post