" MR. BLACK ZANZIBAR, AKUTANA NA WAZIRI WA UTAMADUNI KUELEKEA SUKUMA FESTIVAL ZANZIBAR

MR. BLACK ZANZIBAR, AKUTANA NA WAZIRI WA UTAMADUNI KUELEKEA SUKUMA FESTIVAL ZANZIBAR


Muandaaji wa Shinyanga Sukuma Festival kupitia kampuni ya The BSL Investments Company Limited, Peter Frank Lugumi maarufu kama Mr. Black, amekutana na Waziri wa Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Riziki Pembe, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndugu Mattar Zahoro, katika hatua za awali za maandalizi ya kupeleka Tamasha la Utamaduni wa Wasukuma Zanzibar.Katika kikao hicho, Mr. Black na viongozi hao wamefanya mazungumzo ya awali kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa Sukuma Festival Zanzibar, ikiwemo maandalizi ya tamasha hilo katika maeneo ya fukwe za Zanzibar, kwa lengo la kuendeleza utamaduni wa Kisukuma na kuufikisha katika hadhira pana zaidi ndani na nje ya Tanzania.Shinyanga Sukuma Festival imeendelea kukua na kupata umaarufu katika miaka ya hivi karibuni, huku Mr. Black kupitia The BSL Investments Company Limited akiendelea kulikuza na kulitangaza tamasha hilo kitaifa na kimataifa kama jukwaa la kuhifadhi, kuendeleza na kuutangaza utamaduni wa Wasukuma pamoja na fursa zinazotokana na sanaa, utamaduni na ubunifu.Mazungumzo hayo ya awali pamoja na mapokezi yaliyotolewa na Wizara ya Habari, Sanaa, Michezo na Utamaduni Zanzibar yanafungua milango mipya ya ushirikiano wa kitamaduni ndani ya Muungano wa Tanzania, hususan katika eneo la utunzaji, uendelezaji na utangazaji wa utamaduni wa Tanzania kimataifa.Waziri Mh. Riziki Pembe pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara, Ndugu Mattar Zahoro, wameeleza utayari wa Wizara kutoa ushirikiano katika hatua mbalimbali za maandalizi na kuendelea kuwakaribisha wadau wa utamaduni kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kutembelea na kushirikiana na Zanzibar katika kukuza sekta ya utamaduni.Kwa upande wake, Mr. Black ametoa shukrani kwa uongozi wa Wizara kwa mapokezi na utayari wa kushirikiana, akieleza kuwa mazungumzo hayo ni hatua muhimu katika kufungua ukurasa mpya wa Sukuma Festival Zanzibar na kuahidi kuendelea kufanya juhudi zaidi kuhakikisha maandalizi ya tamasha hilo yanafikia viwango vya kitaifa na kimataifa.Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuifanya Shinyanga Sukuma Festival kuwa jukwaa la kuunganisha jamii, utamaduni na fursa za kiuchumi, huku ikitoa nafasi kwa utamaduni wa Kisukuma kufahamika zaidi ndani na nje ya Tanzania.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post