
Wananchi wa Kata ya Jilailai, Wilaya ya Longido Mkoani Arusha wamekubali uanzishaji wa mradi wa madini ya magadi katika Ziwa Natron kufuatia ufafanuzi uliotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao Oktoba 11, 2026, Diwani wa Kata hiyo Simon Waiteswi amesema ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu, Dkt. Richard Muyungi umerejesha matumaini na imani ya wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.
Amesema wananchi hao wameridhishwa na ufafanuzi wa Serikali kuhusu manufaa ya mradi ambao unaolenga kuboresha miundiombinu ya huduma za kijamii na kiuchumi ikiwemo elimu, maji, afya na barabara.
“Wananchi wamefurahi na maelezo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi kuhusu mradi huu ambao utakuja kuboresha huduma za maji, elimu, afya, barabara sambamba na ujenzi wa majosho na malambo ya mifugo” amesema Waiteswi.
Amesema awali wananchi wa vijiji vinavyotarajia kutekeleza mradi huo ambavyo ni Wosiwosi, Alaililai, Ilchang’t sapukin walipata hofu ya kupoteza ardhi yao na hivyo kuhitaji ufafanuzi wa Serikali na mwekezaji kuhusu manufaa ya mradi na kufahamu vipimo halisi vya ramani ya maeneo ya utekelezaji.
Amesema mwekezaji wa mradi huo kampuni ya Soda Ash Ltd alifika katika Kata hiyo na kuzungumza na Viongozi wa Serikali za Vijiji na wananchi ambapo hoja mbalimbali zilibuiliwa na wananchi lakini zilishindwa kupatiwa ufafanuzi wa kina kuhusu mradi huo.
“Ufafanuzi huu uliotolewa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais umewatoa hofu wananchi na sasa wapo tayari kuona mradi huu unaanza kutekelezwa na wapo tayari kushirikiana na mwekezaji” amesema Waiteswi.
Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi aliwatoa hofu wananchi wa vijiji vinavyotarajia kunufaika na mradi huo na kuwaeleza kuwa hakuna mwananchi atakayehamishwa na kuchukuliwa ardhi yake na pia eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi huo ni ekari 150 pekee.
Ameongeza kuwa Ziwa Natroni lina ukubwa wa mita za mraba 2114 ambapo eneo linalotarajia kutumia kwa ajili ya shughuli za utekelezaji wa mradi ni asilimia 4 pekee huku asilimia 96 iliyobaki itaendelea kutumika katika shughuli nyinginezo za kijamii na kiuchumi.
Amesema mradi huo umekuja kwa wakati mwafaka kwani unatarajia kuleta manufaa kwa jamii na wananchi wa eneo hilo ikiwemo upatikanaji wa ajira na uimarishaji wa huduma za miundombinu ya kijamii ikiwemo maji, elimu na barabara.
Amesema ziara yake imelenga kujionea uhalisia wa mradi sambamba na kupokea ushauri, maoni na mapendekezo ya wananchi kabla ya Ofisi yake haijachukua hatua ya kuruhusu utekelezaji wa mradi huo.
“Serikali ipo pamoja na wananchi na hivyo nahimiza Halmashauri ya Wilaya kushirikiana na mwekezaji kuhakikisha suala la elimu kuhusu manufaa ya mradi huu inatolewa kwa wananchi” amesema Dkt. Muyungi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mwekezaji wa mradi huo kutoka kampuni ya Soda Ash Ltd, Yesaya Kaoneka amesema kampuni hiyo imepokea maoni na ushauri uliotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na viongozi wa Serikali za vijiji na kuahidi kufanyia kazi.
“Tumepokea maoni na ushauri uliotolewa na pia tumefurahishwa kuona viongozi wa serikali na wananchi na mradi walivyoshirikiana” amesema Kaoneka.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais aliambatana pia na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini, Benjamin Dotto.


PROFESSOR MGOKO EPISODE 05
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 09
Post a Comment