Zaidi ya abiria 40 wamenusurika kifo baada ya basi la abiria mali ya Kampuni ya Usafirishaji ya Abood kuteketea kwa moto katika eneo la Isaka, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

Basi hilo lenye namba za usajili T 285 EAV, lilikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea mkoani Kagera lilipokumbwa na tukio hilo la moto leo, Novemba 13, 2026, majira ya saa 11 alfajiri.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, SSP Stanley Luhwago, amesema kikosi cha zimamoto kilipata taarifa na kufika eneo la tukio, ambapo kilifanikiwa kuudhibiti na kuuzima moto huo.

Kutokana na tukio hilo, abiria wote waliokuwamo ndani ya basi hilo wameelezwa kunusurika, huku basi hilo likiteketea kwa moto.

Chanzo cha moto huo na thamani ya mali iliyopotea bado havijaelezwa.