" TAKUKURU SHINYANGA YAREJESHA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 236 KWA MIEZI SITA

TAKUKURU SHINYANGA YAREJESHA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 236 KWA MIEZI SITA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kurejesha jumla ya Shilingi 236,069,957.63 katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, kupitia udhibiti wa makusanyo ya mapato ya ndani, ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma, uchunguzi na mashtaka.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, amesema fedha hizo zimepatikana kupitia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na taasisi hiyo katika maeneo tofauti ya mkoa huo.

Amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 75,500,500 zimeokolewa baada ya ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za kielektroniki za POS katika mnada wa Old Shinyanga, unaosimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, ambapo ilibainika kuwa baadhi ya mawakala walikusanya fedha za ushuru lakini hawakuzifikisha benki kwa wakati kama taratibu zinavyotaka.

Aidha, Shilingi 47,877,360 zimeokolewa baada ya TAKUKURU kufuatilia malipo ya wakulima wa pamba katika msimu wa 2025/2026, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ambapo kulikuwa na sintofahamu ya malipo ya wakulima licha ya kampuni zilizopewa vibali vya kununua pamba kukabidhi fedha kwa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).

Katika hatua nyingine, taasisi hiyo imefanikisha ukusanyaji wa Shilingi 35,129,844.63 kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kutoka kwa wadaiwa sugu wa ushuru wa huduma (Service Levy) waliokuwa wamekwepa kulipa kwa muda mrefu.

Katika eneo la ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika mradi wa ujenzi wa miundombinu mipya katika Zahanati ya Mwakitolyo, unaohusisha jengo la upasuaji na jengo la wazazi wenye thamani ya Shilingi milioni 250.

Masanja amesema ufuatiliaji huo ulibaini kutowasilishwa kwa baadhi ya malipo ya kodi ya zuio (Withholding Tax), ambapo baada ya uchunguzi wa kina kiasi cha Shilingi 2,692,139 kililipwa.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho, TAKUKURU Shinyanga imefuatilia matumizi ya fedha katika miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 27.9 katika sekta za elimu, afya, barabara, huduma za jamii na utawala.

Kuhusu elimu kwa umma, amesema taasisi hiyo imeendelea kuishirikisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia klabu 100 za wapinga rushwa, semina 44, mikutano ya hadhara 41, maonesho 14, uandishi wa habari na makala saba pamoja na vipindi saba vya redio.

Katika upande wa uchunguzi na mashtaka, Masanja amesema TAKUKURU Shinyanga imefanikisha kurejeshwa Serikalini kwa Shilingi 74,870,114 zilizotokana na uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa mali za umma, baada ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani na kukiri makosa yao.

Amesema katika kipindi hicho jumla ya malalamiko 134 yalipokelewa, ambapo 105 yalihusu rushwa na 29 hayakuhusu rushwa. Malalamiko yaliyohusu rushwa yameanzishiwa uchunguzi na yanaendelea kushughulikiwa katika hatua mbalimbali.

Aidha, kesi 13 ziliendelea mahakamani, huku kesi mpya saba zikifunguliwa, kesi saba zikitolewa uamuzi na Jamhuri kushinda kesi sita.

Akizungumzia mikakati ya kipindi kinachofuata, Masanja amesema TAKUKURU itaendelea kuimarisha elimu kwa umma katika maeneo ya utoaji huduma, kufuatilia matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo, kusimamia makusanyo ya mapato ya ndani na kuimarisha uadilifu katika taasisi za umma.

Amewataka wananchi na taasisi za umma mkoani Shinyanga kuzingatia misingi ya uadilifu na maadili ya kazi, huku akihimiza wananchi kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ili kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haki.

Wananchi wenye taarifa za vitendo vya rushwa wametakiwa kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizo karibu nao au kupiga simu ya bure namba 113.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post