Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameelekeza
kuwasilishwa kwa maombi ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika Jimbo la
Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, pamoja na hatua za kuajiri walimu
wawili waliojitolea katika Shule ya Msingi Masunula baada ya shule hiyo kufanya
vizuri katika matokeo ya kitaifa.
Maelekezo
hayo ameyatoa leo Novemba 10, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Singita, Kata ya Usanda, Jimbo la
Itwangi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, aliwasilisha hoja mbalimbali zinazohusu mahitaji ya wananchi wa jimbo hilo, ikiwemo uhitaji wa vituo viwili vya afya katika Kata za Usule na Didia, pamoja na changamoto ya kutokukamilika kwa jengo la Zahanati ya Mwamkanga.
Katika hoja zake, Mbunge huyo pia alieleza umuhimu wa walimu wawili wa kujitolea wa Shule ya Msingi Masunula kupata ajira serikalini, akizingatia mchango wao katika shule hiyo iliyofanya vizuri na kushika nafasi ya pili kitaifa.
Dkt. Mwigulu
amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kuandaa na kuwasilisha maombi ya
ujenzi wa vituo viwili vya afya katika Kata za Usule na Didia ili kusaidia
kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa maeneo hayo.
Aidha,
Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kutoa ahadi ya kutafuta Shilingi milioni 76
kwa ajili ya kukamilisha jengo la Zahanati ya Mwamkanga, ili wananchi wa eneo
hilo waanze kupata huduma za afya karibu na maeneo yao.
Katika sekta
ya elimu, Dkt. Mwigulu ameelekeza walimu wawili wa kujitolea waliokuwa
wakifundisha katika Shule ya Msingi Masunula waajiriwe na Serikali kutokana na
mchango wao katika kuifanya shule hiyo kufanya vizuri na kushika nafasi ya pili
kitaifa.
Amesema
hatua hiyo inalenga kutambua mchango wa walimu hao ambao wamekuwa wakijitolea
kwa zaidi ya miaka mitano, licha ya changamoto ya upungufu wa walimu shuleni
hapo.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amepokea ombi la wananchi wa Jimbo la Itwangi la kutaka
eneo hilo kuwa na Halmashauri inayojitegemea, tofauti na hali ya sasa ambapo
linaendelea kuwa sehemu ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Akijibu ombi
hilo, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imelipokea na kuelekeza viongozi na
watendaji kuanza kukamilisha huduma na miundombinu ya msingi inayohitajika ili
eneo hilo liweze kufikia vigezo vya kuanzishwa kwa Halmashauri yake.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema mkoa huo umepokea
jumla ya Shilingi trilioni 2.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema
fedha hizo zimeelekezwa katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, maji,
barabara, nishati na miundombinu mingine ya kijamii na kiuchumi, hatua
inayolenga kuboresha huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya mkoa huo.
Mkutano huo
pia umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Andrea Mathew Kundo,
pamoja na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar R. Seif, ambao wameshiriki katika shughuli za
mkutano huo pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Ziara ya
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba mkoani Shinyanga inaendelea, ambapo kesho atafanya
mikutano ya hadhara katika Halmashauri ya Ushetu Pamoja na Msalala.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi wa Jimbo la Itwangi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Singita, Wilaya ya Shinyanga, Novemba 10, 2026.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akieleza mafanikio ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa mkoani humo, akisema jumla ya Shilingi trilioni 2.2 zimepokelewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akiwasilisha hoja na kueleza mahitaji ya wananchi wa jimbo hilo mbele ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Singita, Wilaya ya Shinyanga, Novemba 10, 2026.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Jafar R. Seif, akifuatilia mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba katika Jimbo la Itwangi.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Andrea Mathew Kundo, akiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba na wananchi wa Jimbo la Itwangi.
Wananchi wa jimbo la Itwangi wakifuatilia hotuba ya waziri mkuu.
PROFESSOR MGOKO EPISODE 07
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254





























Post a Comment