Issa Mbande mratibu wa Baba,Mama na mtoto wilaya ya Chunya
Na Lydia Lugakila,Misalaba media
Chunya/Mbeya.
Jamii wilayani Chunya imetakiwa kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, huku wanaume wakihimizwa kushiriki kikamilifu katika malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya watoto badala ya kuwaachia wanawake jukumu hilo.
Wito huo umetolewa kupitia utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu malezi bora na kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye afya.
Kupitia programu hiyo, elimu hutolewa katika majukwaa mbalimbali ya kijamii, mabonanza ya michezo na vituo vya kutolea huduma za afya, ikijikita katika masuala ya lishe, afya, ulinzi, usalama na maendeleo ya mtoto.
Akizungumza Novemba 2, 2026, wakati wa kikao cha kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za robo ya kwanza kuanzia Julai hadi Septemba, kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya, Afisa Ustawi wa Jamii, Luthness Mbisa, amewasisitiza wajumbe kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi.
Mbisa amesema malezi ya mtoto ni jukumu la pamoja linalohusisha baba, mama na jamii nzima, hivyo ni muhimu kila mmoja kutambua wajibu wake katika kuhakikisha mtoto anapata malezi yanayostahili.
Christina Jahari Afisa ustawi.
Kwa upande wao, Christina Jahari, Issa Mbande na Jamila Kimaro, wakati wa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali, wamesema elimu ya malezi na makuzi ya mtoto imeendelea kutolewa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, majukwaa ya kijamii, mabonanza ya michezo pamoja na vikundi mbalimbali vilivyopo katika jamii.
Jamila Kimaro Afisa lishe.
Aidha, kikao hicho kimeazimia kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wanaume ili washiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto kwa kutumia njia mbalimbali zinazolenga kuongeza uelewa na ushiriki wao.
Katika hatua nyingine, wanaume wamehamasishwa kuambatana na wenza wao katika vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa ujauzito ili kupata elimu, ushauri na vipimo muhimu kwa ajili ya kulinda afya na usalama wa mama pamoja na mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inahusisha wadau kutoka idara mbalimbali, zikiwemo Idara ya Afya, Maendeleo ya Jamii na Idara ya Elimu ya Awali na Msingi, kwa lengo la kuimarisha uratibu na utekelezaji wa shughuli za malezi na makuzi ya watoto katika jamii.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment