" KAMENGE ATOA SOMO KWA WAHITIMU KIGARAMA, ASEMA AJIRA ZIPO KWENYE FURSA

KAMENGE ATOA SOMO KWA WAHITIMU KIGARAMA, ASEMA AJIRA ZIPO KWENYE FURSA



Na Lydia Lugakila Misalaba media,Missenyi /Kagera

Dhana ya kusubiri ajira baada ya kuhitimu masomo imeelezwa kuwa kikwazo kwa baadhi ya vijana kujikwamua kiuchumi, huku wakihimizwa kutambua na kutumia fursa zinazowazunguka kujitengenezea ajira na kipato.

Mchumi na mkulima kutoka mkoani Kagera, Evance Kamenge, ametoa somo hilo kwa wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Kigarama, iliyopo Kata ya Kanyigo, Wilaya ya Missenyi, akiwataka kutumia elimu waliyoipata shuleni kuwa msingi wa kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa.

Akizungumza katika mahafali ya 24 ya shule hiyo yaliyofanyika Oktoba 31, 2026, Kamenge amesema dunia ya sasa imejaa fursa ambazo vijana wanaweza kuzitumia kujenga maisha yao, kuimarisha uchumi wa familia na kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema wahitimu hawapaswi kukaa bila shughuli za uzalishaji mali wanaposubiri matokeo yao, bali waanze na miradi midogo inayoweza kuleta kipato, ikiwemo kilimo cha mboga za majani na ufugaji wa kuku.

Ameeleza kuwa maarifa ya ujasiriamali waliyopata wakiwa shuleni yanapaswa kutafsiriwa katika vitendo kwa kutambua changamoto zilizopo katika jamii na kuzigeuza kuwa fursa za kiuchumi.

Katika kusisitiza umuhimu wa kutumia fursa hizo, Kamenge ameitaja sekta ya viwanda vidogo vya kuchakata mazao na kutengeneza chakula cha mifugo kuwa miongoni mwa maeneo yenye uwezekano wa vijana kuwekeza na kujitengenezea ajira.

Kamenge amebainisha kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo mengi ya mkoani Kagera unaweza kuwa kichocheo cha kuanzishwa kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji na uchakataji wa bidhaa.

Aidha, amewataka wahitimu hao kuwa na ubunifu, kuthubutu na kujituma, akisisitiza kuwa fursa za kujikwamua kiuchumi hazipaswi kusubiriwa, bali zinahitaji kutambuliwa na kutumiwa ipasavyo.

Mbali na kuwahimiza kujiajiri, Kamenge amewataka wahitimu hao kuendelea kudumisha nidhamu na maadili mema wanaporejea katika jamii, ili kuwa mabalozi wazuri wa shule yao wakati wakisubiri matokeo.

Amesema kuhitimu Kidato cha Nne ni mwanzo wa safari nyingine ya maisha, hivyo wanapaswa kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila hatua wanayopiga.

Wakati huohuo, amewakumbusha wazazi kuendelea kuwaombea watoto wao, kuwashauri na kuwaongoza katika njia sahihi ili waweze kufanya maamuzi yatakayowajenga na kuwasaidia kufikia malengo yao.

PROFESSOR MGOKO EP 07

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post