Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikiwa kukamata silaha 105, kutibua mitego 1,971 ya ujangili na kukamata mifugo 65,600 iliyokuwa ikiingia ndani ya hifadhi za taifa kinyume cha sheria katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Aidha, shirika hilo limeimarisha udhibiti wa migogoro baina ya binadamu na wanyamapori kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo ndege zisizo na rubani (drones), mifumo ya GPS na vituo vya mawasiliano vinavyosaidia kufuatilia mienendo ya wanyamapori na kuwazuia kuingia katika maeneo ya wananchi.
Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa, amesema hayo Novemba 10, 2026, wakati akizungumza katika kikao kazi na wahariri kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), kilichofanyika katika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam.
Mwishawa amesema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha uhifadhi, kulinda rasilimali za wanyamapori na kuhakikisha sekta ya utalii inachangia maendeleo ya taifa.
Amesema TANAPA imeimarisha shughuli za doria na ulinzi katika hifadhi za taifa, ambapo katika kipindi hicho imefanya doria 31,314 dhidi ya 14,940 zilizokuwa zimepangwa, hatua iliyosaidia kukabiliana na ujangili na vitendo vingine vinavyohatarisha rasilimali za taifa.
“Tumekamata watuhumiwa wa ujangili 385 katika matukio mbalimbali na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi. Lengo ni kuhakikisha uhalifu huo unadhibitiwa na rasilimali zetu zinaendelea kulindwa,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ulinzi wa hifadhi, ikiwemo upatikanaji wa ndege zisizo na rubani 40 zinazotumika kufanya doria za angani, kufuatilia mienendo ya wanyamapori na kusaidia askari kubaini maeneo yenye viashiria vya uhalifu.
Amesema shirika hilo pia limeweka mifumo ya GPS kwa baadhi ya wanyamapori ili kufuatilia mienendo yao na kutoa taarifa mapema wanapokaribia maeneo ya wananchi, hatua inayosaidia kupunguza madhara yanayotokana na migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Mwishawa amesema TANAPA imejenga vituo vitatu vya kisasa vya mawasiliano katika Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere, vinavyosaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za ulinzi na usalama.
Amesema shirika hilo linaendelea kuimarisha mifumo ya mawasiliano ya redio katika hifadhi mbalimbali, ikiwemo Serengeti, Ziwa Manyara, Tarangire, Mkomazi na Nyerere, ili kurahisisha mawasiliano kati ya askari na vyombo vingine vya usalama.
Katika hatua nyingine, amesema TANAPA imeendelea kurejesha mifumo ikolojia iliyoharibiwa na shughuli zisizo endelevu, ikiwemo kudhibiti mimea vamizi katika hekta 984.2 za hifadhi 15 na kusafisha hekta 1,546 zilizokuwa zimeathirika na vichaka katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Amesema hatua hiyo inalenga kurejesha maeneo ya malisho ya wanyamapori na kuboresha mazingira yao, huku ikisaidia kukabiliana na changamoto ya wanyama kutoka hifadhini kwenda katika maeneo ya wananchi kutafuta malisho.
Mwishawa amesema TANAPA pia imefanikiwa kurejesha ukanda wa ikolojia unaounganisha Hifadhi za Taifa za Katavi na Milima Mahale kwa kushirikiana na wananchi, ambapo eneo hilo limeendelea kuhifadhi misitu ya asili na kuwa njia ya wanyamapori kuhama kati ya hifadhi hizo.
Amesema kupitia mradi huo, wananchi wanaozunguka eneo hilo wananufaika na shughuli za kiuchumi, ikiwemo biashara ya hewa ukaa na mikataba inayowezesha kupata mapato kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi.
Katika suala la maendeleo ya jamii, Kamishna huyo amesema TANAPA imeendelea kushirikisha wananchi wanaozunguka hifadhi katika shughuli za uhifadhi na miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa zahanati, madarasa, nyumba za walimu, miundombinu ya maji na barabara.
Amesema shirika hilo pia linaendelea kutoa ajira kwa Watanzania, hususan vijana wanaotoka katika maeneo yanayozunguka hifadhi, huku likitengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji wa sekta ya utalii ili kuongeza fursa za ajira kupitia hoteli, usafirishaji na huduma nyingine za utalii.
Mwishawa amesisitiza kuwa TANAPA itaendelea kushirikiana na jamii, taasisi za Serikali na wadau wengine kuhakikisha uhifadhi unakuwa endelevu na wenye manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

PROFESSOR MGOKO EP 07
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment