" WANAFUNZI 90 WA TANZANIA WATUA ALGERIA πŸ‡ΉπŸ‡ΏπŸ‡©πŸ‡Ώ

WANAFUNZI 90 WA TANZANIA WATUA ALGERIA πŸ‡ΉπŸ‡ΏπŸ‡©πŸ‡Ώ

​Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amewataka wanafunzi wa Tanzania waliowasili nchini Algeria kusoma kwa juhudi na bidii wakitambua kwamba wao ni ndoto na fahari ya Taifa.

​Akizungumza na wanafunzi hao mnamo tarehe 25 Novemba, 2026, kwenye Chuo Kikuu cha Blida kilichopo kilomita 45 kutoka Algiers wakati wakijiandaa kuelekea vyuoni mwao, Balozi Matinyi aliwasisitizia kuishi kama ndugu wakikumbuka kwamba wanaibeba heshima ya Tanzania na Programu ya Ufadhili ya Samia.

​“Tambueni kwamba mnaibeba heshima ya nchi yetu kupitia Samia Scholarship ambayo ni alama ya heshima ya ubora kitaaluma,” alisema Balozi Matinyi ambaye alikuwa ameambatana na viongozi wa Chuo Kikuu cha Blida na ujumbe wa Serikali kutoka Tanzania.

​Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Blida, Prof. Bachir Amer, aliwasilisha salamu toka kwa Waziri wa Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi wa Algeria, Prof. Kamel Bidari, kwa Balozi Matinyi, ujumbe wa Serikali na wanafunzi wa Tanzania.

​Kiongozi wa msafara uliowaleta wanafunzi hao ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Steven Maluka, alisema: “Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kugharamia kundi kubwa la wanafunzi bora 90 kwenda nje ya nchi kusomea shahada za sayansi na teknolojia.”

​Aidha, Prof. Maluka aliungana na Balozi Matinyi kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zilizowezesha wanafunzi hawa kupata fursa za elimu ya juu katika fani za sayansi na teknolojia nchini Algeria.

​Ujumbe wa Serikali uliowasindikiza wanafunzi hao uliwajumuisha pia Afisa Mwandamizi wa Wizara, Dkt. Fabian Nyenyembe, na Mratibu wa Samia Scholarship, Prof. Liliane Pasape, kutoka Chuo Kikuu cha Afrika cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) kilichopo Arusha.

​Wanafunzi hao waliwasili nchini Algeria jioni ya tarehe 24 Novemba, 2026, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar na kupokelewa na Balozi Matinyi, maofisa wa Ubalozi na watendaji wa Wizara ya Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi ya Algeria kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumedienne, jijini Algiers.

​Wanafunzi hao ambao wanakwenda kusomea masomo ya afya, sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, wamegawanywa na Wizara ya Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi ya Algeria katika vyuo vikuu bora nchini Algeria kwa kuzingatia kiwango chao cha juu cha ufaulu wao nchini Tanzania.

​Vyuo vikuu hivyo vilivyopokea wanafunzi wa Tanzania ni Algiers, Annaba, Batna, Blida, Boumedienne, Boumerdes, Chlef, Constantine, Mostaganem, Oran, Setif, Sidi Bel Abbes, Skikda na Tiaret. Aidha, mbali ya masomo yao wanatarajia pia kujifunza lugha za kimataifa za Kifaransa au Kiarabu.


​#Tanzania #Algeria #SamiaScholarship #ElimuYaJuu #SayansiNaTeknolojia #Habari #DktSamiaSuluhuHassan





Post a Comment

Previous Post Next Post