" JE UNATAKA KUFUGA SAMAKI?, ROFACOL TANZANIA YAKUPATIA VIFARANGA BORA, CHAKULA NA UJENZI WA MABWAWA

JE UNATAKA KUFUGA SAMAKI?, ROFACOL TANZANIA YAKUPATIA VIFARANGA BORA, CHAKULA NA UJENZI WA MABWAWA

Na Lydia Lugakila- Misalaba Media

MBEYA

KATIKA jitihada za kukuza uchumi wa buluu na kuwapatia vijana fursa za kujiajiri, kampuni ya ROFACOL Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa wadau wanaotoa huduma mbalimbali za ufugaji wa samaki, ikiwemo uzalishaji na uuzaji wa vifaranga vya samaki aina ya Sato na Kambale, ujenzi wa mabwawa, chakula cha samaki pamoja na elimu ya lishe na namna bora ya kuendesha miradi ya ufugaji wa samaki.

Kampuni hiyo inayomilikiwa na familia na inayopatikana katika Kata ya Inyala, Kijiji cha Shamwengo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, imekuwa ikitoa fursa kwa vijana kupata maarifa na ujuzi wa ufugaji wa samaki, huku ikilenga kuongeza uzalishaji wa vifaranga bora na kusaidia wananchi kujiongezea kipato kupitia shughuli hiyo.

Akizungumza na Misalaba Media, mwanzilishi wa mradi huo, Mary Francis Misinzo, amesema wazo la kuanzisha biashara hiyo lilitokana na changamoto ya ajira aliyoikabili baada ya kuhitimu Shahada ya Sayansi ya Viumbe wa Majini katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Amesema baada ya kuhitimu mwaka huo, aliamua kutumia taaluma yake kujiajiri badala ya kusubiri ajira, hatua iliyomfanya kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki mwaka 2016 akiwa eneo la Kiwira, wilayani Rungwe, ambako alianza kwa kukodi mabwawa.

Misinzo amesema katika hatua za mwanzo alifanya utafiti wa mazingira yanayofaa kwa ufugaji wa samaki na kubaini kuwa maeneo ya Rungwe yalikuwa na changamoto ya hali ya hewa ya baridi, hivyo kuamua kuhamishia shughuli zake Mbeya Vijijini kutokana na mazingira na joto linalofaa zaidi kwa shughuli hiyo.

Amesema baada ya kufika Kijiji cha Shamwengo alibaini uwepo wa mabwawa mengi, yanayokadiriwa kufikia 200, na kushirikiana na Afisa Uvuvi aliyemwelekeza fursa zilizokuwepo katika eneo hilo.

Hatua hiyo ilimuwezesha kukodi mabwawa mawili kwa ajili ya kufuga samaki aina ya Sato na Kambale, huku mbegu za awali akizipata kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Morogoro.

Amesema mradi huo umekuwa msingi wa maendeleo yake na familia yake, kwani mbali na kuendeleza ufugaji wa samaki, ameweza kujihusisha na shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji wa kuku, pamoja na kusaidia kusomesha watoto na kutoa ajira kwa vijana.

Akielezea shughuli za uzalishaji, Misinzo amesema kwa sasa mradi wake una jumla ya mabwawa manne yenye matumizi tofauti katika mchakato wa ufugaji na uzalishaji wa vifaranga.

Amesema bwawa la kwanza lina samaki wazazi aina ya Sato wapatao 6,000, ambao kwa makadirio wana uwezo wa kuzalisha vifaranga 25,000 ndani ya wiki mbili.

Ameongeza kuwa bwawa la pili lina samaki aina ya Kambale wapatao 3,000, ambao wanatarajiwa kufikia hatua ya uzalishaji wa mayai baada ya miezi sita.

Kwa upande wa bwawa la tatu, amesema hutumika kwa ajili ya majaribio na maonesho ya uzalishaji kwa wateja wanaotembelea mradi huo kujifunza kabla ya kununua vifaranga, huku bwawa la nne likitumika maalumu kwa kuhifadhi vifaranga.

Katika kuunga mkono jitihada za serikali za kupunguza changamoto ya ajira, Misinzo amesema tayari vijana watatu wamenufaika na mradi huo kwa kupata mafunzo ya vitendo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za ufugaji wa samaki.

Amesema vijana hao wamefundishwa namna ya kupima mazingira ya mabwawa, ujenzi wa mabwawa, usafi, utunzaji wa samaki, ukadiriaji wa vifaranga na taratibu za uzalishaji.

Ameeleza kuwa mbali na kupata ujuzi, vijana hao wanashiriki katika shughuli za mradi na kulipwa kulingana na mapato yanayopatikana.

Misinzo amesema lengo lake ni kupanua wigo wa mafunzo hayo kwa kuwafikia vijana wasiopungua 100 ili kuwajengea uwezo wa kuanzisha miradi yao na kujipatia kipato badala ya kuendelea kusubiri ajira.

Hata hivyo, amesema bado anakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa baadhi ya vifaa muhimu vya uzalishaji, hususan nyumba maalumu ya kuzalishia vifaranga ambayo itasaidia kuendeleza uzalishaji katika mazingira tofauti ya hali ya hewa, ikiwemo kipindi cha baridi, joto na mvua.

Amesema eneo hilo lina maji ya kutosha na mazingira yanayofaa kwa ufugaji wa samaki, hivyo anaomba serikali na wadau mbalimbali kumuunga mkono ili aweze kuongeza uzalishaji na kupanua huduma za mafunzo kwa vijana.

Aidha, amewaomba wadau wenye maeneo yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kushirikiana naye kwa kutoa maeneo hayo ili yaweze kutumika katika uzalishaji na kuwafikia vijana wengi zaidi.

Amesema kuna wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa mito na wenye mazingira yanayofaa kwa ufugaji wa samaki, lakini bado hawajatumia fursa hiyo kutokana na kukosa elimu na uelewa wa kutosha kuhusu shughuli hiyo.

Amesisitiza kuwa ufugaji wa samaki ni fursa inayoweza kumsaidia mwananchi kuongeza kipato cha familia yake ikiwa atapata elimu sahihi na kuitumia vizuri.

Misinzo amesema anatamani kuona ROFACOL Tanzania inakua na kuwa kampuni kubwa ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za samaki nchini, ili kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi na kukidhi mahitaji ya soko.

Amesema tayari amepata fursa ya kushiriki katika semina mbalimbali zinazohusu ufugaji wa samaki na maendeleo ya sekta hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar, ambazo zimemsaidia kuongeza maarifa na kubadilishana uzoefu na wadau wengine.

Ameeleza kuwa wateja wake wanatoka maeneo mbalimbali ikiwemo Mwanza na Ludewa, huku akilenga kupanua huduma zake zaidi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Songea, Iringa na Njombe.

Ameongeza kuwa moja ya matarajio yake ni kuongeza uwezo wa kuzalisha na kusambaza vifaranga vingi kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya wateja na kufikia malengo ya kampuni kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Misinzo ameipongeza serikali kwa kuendeleza kampeni ya uchumi wa buluu, akisema imeongeza mwamko na kuwafanya wadau mbalimbali kuanza kutambua fursa zilizopo katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki.

Amesema kupitia mwamko huo amekuwa akipokea mawasiliano kutoka kwa wadau na wateja wanaohitaji vifaranga vya samaki, jambo linaloonesha kuwa sekta hiyo ina nafasi kubwa ya kuchangia uchumi wa wananchi.

Amewataka vijana wenye taaluma mbalimbali ikiwemo kilimo na udaktari kutokujifungia katika ajira zinazohusiana moja kwa moja na taaluma zao pekee, bali wawe tayari kuchunguza fursa nyingine za kujiajiri zinazopatikana katika jamii.

Amewasisitiza kutokata tamaa wanapokutana na changamoto za maisha, akieleza kuwa elimu waliyoipata inaweza kutumika kubuni miradi na kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wa huduma, Misinzo amewataarifu wateja wake wapya na wa zamani kuwa anatarajia kuwa na vifaranga vya samaki mwezi Agosti 2027, ambapo kifaranga kimoja kitauzwa kwa Shilingi 200.

Amewahimiza wananchi wanaotaka kuanzisha au kupanua miradi ya ufugaji wa samaki kuwasiliana naye mapema kwa ajili ya kupata maelekezo na huduma zinazotolewa na ROFACOL Tanzania.

Kwa mawasiliano zaidi, mwanzilishi wa mradi huo, Mary Francis Misinzo, anapatikana kwa namba 0746 414 196.

PROFESSOR MGOKO EPISODE 08

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post