" RED CROSS YATEMBELEA WAHANGA WA MVUA SHINYANGA,KAYA 47 ZAATHIRIKA, WATU WENGINE WAPELEKWA HOSPITALI

RED CROSS YATEMBELEA WAHANGA WA MVUA SHINYANGA,KAYA 47 ZAATHIRIKA, WATU WENGINE WAPELEKWA HOSPITALI

Uongozi mpya wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (Tanzania Red Cross Society) Mkoa wa Shinyanga umetembelea maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha usiku wa Novemba 16, 2026, katika Manispaa ya Shinyanga, kwa lengo la kujionea madhara yaliyotokea na kuwafariji wananchi walioathirika.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika leo Novemba 17, 2026, Mwenyekiti wa Red Cross Mkoa wa Shinyanga, Hatibu Mgeja, amewahimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha, hususan kwa kuhakikisha wanazunguka mazingira ya makazi yao na kubaini vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara.

Amesema baadhi ya nyumba zimeezuliwa mapaa na nyingine kuangukiwa na miti kutokana na upepo mkali, huku akiwashauri wananchi wanaoishi katika nyumba zilizo karibu na miti mikubwa au maeneo yenye miti isiyo salama kuchukua hatua za mapema ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.

Mgeja amewapa pole wananchi wote walioathirika na majanga hayo, akieleza kuwa Red Cross iko tayari kushirikiana na wenyeviti wa mitaa, watendaji, viongozi wa kata na wilaya katika kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na majanga mbalimbali, pamoja na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za tahadhari kabla ya madhara kutokea.

Kwa mujibu wa taarifa ya Red Cross Mkoa wa Shinyanga, shirika hilo limetembelea maeneo matano yaliyoathirika ambayo ni Kata ya Ndembezi eneo la Mazinge ambako kaya sita zimeathirika, kata ya Ibadakuli kaya saba; Bugweto kaya sita, kata ya Kitangili kaya 12 na Masekelo kaya 16 na kufanya jumla ya kaya 47 zilizoathirika na mvua hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya nyumba zimeezuliwa mapaa, huku familia nyingine zikikosa makazi na kulazimika kuhifadhiwa na majirani. Pia, baadhi ya vyakula na vifaa vya ndani ya nyumba vimelowana na kuharibika kutokana na mvua hiyo.

Katika tukio hilo, watu wawili wameangukiwa na tofali na kujeruhiwa, ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo hadi sasa wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Red Cross imeendelea kuhimiza wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kwa kuimarisha usalama wa makazi yao na kutoa taarifa kwa viongozi wa maeneo yao wanapoona mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha na mali.


PROFESSOR MGOKO EPISODE 07

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post