" KAMATI YA UTEKELEZAJI JUMUIYA YA WAZAZI CCM MPANDA YAPOKEA SHILINGI 500,000 KWA AJILI YA UPIMAJI WA ENEO LA SHULE YA MILALA

KAMATI YA UTEKELEZAJI JUMUIYA YA WAZAZI CCM MPANDA YAPOKEA SHILINGI 500,000 KWA AJILI YA UPIMAJI WA ENEO LA SHULE YA MILALA

Ndg. Pius M. Buzumalle, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo pamoja na Ndg. Heliuth Henry Mbilinyi maarufu Makete CH, Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Uchumi, Mipango na Fedha, baada ya kikao kilichojadili mipango na mikakati ya maendeleo ya Jumuiya hiyo.

Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda imepokea kiasi cha Shilingi 500,000 kutoka kwa Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Uchumi, Mipango na Fedha ya Jumuiya hiyo, Heliuth Henry Mbilinyi maarufu Makete CH, kwa ajili ya kuchangia zoezi la upimaji wa eneo la Shule ya Sekondari na Ufundi Milala.

Fedha hizo zimekabidhiwa leo Novemba 14, 2026, katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Pius M. Buzumalle, kilicholenga kujadili maendeleo ya mpango wa upimaji wa eneo la shule hiyo iliyopo Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi.

Akikabidhi fedha hizo, Mbilinyi amesema mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuhakikisha eneo la shule linapimwa na kupata hati miliki, hatua inayolenga kuweka msingi wa maendeleo ya shule hiyo na kuendeleza elimu katika eneo hilo.

Aidha, amewahimiza wadau mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Mpanda kujitokeza kuchangia juhudi za kuendeleza Shule ya Sekondari na Ufundi Milala, akieleza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha upimaji wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Pius M. Buzumalle, amemshukuru Mbilinyi kwa mchango huo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha umuhimu wa wadau kushiriki kwa vitendo katika juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mahitaji ya shule hiyo.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Jimotoli Jilala Maduka, ameshiriki katika zoezi la kupokea fedha hizo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wadau na viongozi mbalimbali ili washiriki katika juhudi za kuendeleza shule hiyo.

Katika kikao hicho, wajumbe wameeleza kufurahishwa na mchango huo na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza kwa hali na mali ili kusaidia kufanikisha upimaji wa eneo la Shule ya Sekondari na Ufundi Milala na upatikanaji wa hati miliki yake.

Ndg. Pius M. Buzumalle, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, akipokea fedha kiasi cha Shilingi 500,000 kutoka kwa Ndg. Heliuth Henry Mbilinyi maarufu Makete CH, Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Uchumi, Mipango na Fedha ya Jumuiya hiyo, kwa ajili ya kugharamia mchakato wa upimaji wa eneo la Shule ya Sekondari na Ufundi Milala, iliyopo Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi.





Post a Comment

Previous Post Next Post