Jamii imetakiwa kubadilika na kuondoa mtazamo wa kuwaona wanawake kuwa wanafanya makosa, pale wanapochukua hatua ya kwenda kutoa taarifa kwa vyombo mbalimbali, wanapofanyiwa ukatili ndani ya familia .
Rai hiyo imetolewa na Bi.Aisha Omary, ambaye ni Mratibu wa Mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wakati akizungumza kwenye kipindi cha kwanza kinachohusu kuongeza na kukuza mtandao wa kijamii wa kutetea haki za wanawake na watoto, kinachoandaliwa na kurushwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na Women Fund Tanzania Trust (WFT)
Amesema jamii inapaswa kutoendelea kuwashangaa pale wanawake wanapochukua hatua hiyo, na badala yake iwaone kama watu wanaopigania usalama wao na kutafuta nafuu kutokana na magumu wanayopitia, kwa ajili ya maslahi mapana ya familia zao na jamii kwa ujumla.
Mratibu huyo wa MTAKUWWA amebainisha kuwa, kuna madhara makubwa kwa mwanamke anayenyamazia kwa muda mrefu vitendo vya ukatili anavyofanyiwa, kwa kuwa baadaye yeye mwenyewe hugeuka na kuanza kufanya ukatili, kutokana na maumivu ya kisaikolojia anayokaa nayo ndani ya moyo, jambo ambalo linachochea hali ya hasira na kutaka kulipiza kisasi.
Ametolea mfano matukio mengi ya ukatili wanayofanyiwa wanaume na wake zao au watoto na mama zao wa kuwazaa , yanatekelezwa na wanawake ambao wana changamoto ya kisaikolojia na hasira za muda mrefu, kutokana na kunyamazia au kutunza ndani ya moyo maumivu ya ukatili wanaokutana nao.
Ili kuondoa hali hiyo, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa kushirikiana na wadau, inaendelea kutoa elimu kwa wanawake na makundi yote ambayo yamekuwa yakifanyiwa ukatili, ili yatambue aina zote za ukatili na namna ya kupata msaada.
Amewataka wanawake kuacha kasumba ya kunyamazia ukatili wanaofanyiwa ndani ya familia kwa hofu ya kuogopa kuvunja ndoa zao, kwani kuendelea kufanya hivyo kuna madhara makubwa kuliko ndoa wanazozilinda.
Awali wakizungumza na Redio Faraja, baadhi ya wanawake wakazi wa Kata ya Iselamagazi na maeneo jirani wamebainisha kuwa, wamekuwa wakilazimika kukaa kimya pale wanapofanyiwa ukatili kutokana na hali ya hofu iliyojengwa na mifumo ya kijamii, pamoja na kulinda ndoa zao ambazo zimekuwa zikiingia katika mgogoro mkubwa pale wanapoamua kuchukua hatua ya kwenda kuwalalamikia wenzi wao nje ya familia.


Post a Comment