
Shirika
la umoja wa mataifa la kuwasaidia wakimbizi duniani UNHCR, limetoa msaada wenye
thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja kwa wakazi wa kijiji cha
Kagerankanda wilayani Kasulu kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, choo
chenye matundu sita na kuweka mfumo wa maji, anaripoti Respice Swetu - Misalaba Blog.
Akitoa
taarifa ya ujenzi wakati wa hafla ya kukabidhi miundombinu hiyo, mhandisi wa
shirika la UNHCR aliyesimama kazi hiyo Simon Peche ameeleza kuwa jumla ya
shilingi milioni mia moja kumi na mbili, laki tano na ishirini na nane elfu
zimetumika.
Peche
aliyekuwa ameambatana na maafisa wengine wa shirika hilo wakati wa makabidhiano
hayo amesema kuwa, UNHCR kupitia mpango wa kusaidia maeneo yaliyoathiriwa na
wakimbizi, wataendelea kusaidia maeneo hayo kadri itakavyowezekana.
Ameongeza
kuwa msaada kama huo ulioambatana na uwekaji wa madawati kwenye vyumba hivyo,
umefanyika pia katika halmashauri za wilaya ya Kibondo na Kakonko mkoani
Kigoma.
Akipokea
msaada huo kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma, Ofisaelimu taaluma wa
mkoa huo Joas Jonas amelishukuru shirika hilo na kuwataka wakazi wa
Kagerankanda kuyatunza majengo hayo.
"Pamoja
na kuyatunza mnatakiwa kuweka utaratibu wa kuanza kuyatumia mara shule
zitakapofunguliwa Januari mwaka kesho", aliagiza.
Miundombinu
hiyo iliyojengwa kwenye eneo la shule ya msingi ya Nyanzaza iliyoanzishwa zaidi
ya miaka kumi iliyopita, inakusudiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye
shule mama ya Kagerankanda uliotokana na kukosekana kwa madarasa kwenye eneo la
shule ya msingi ya Nyanzaza.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Ofisaelimu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Elestina
Chanafi amesema, kupatikana kwa miundombinu hiyo kutaendeleza ufaulu wa shule
hiyo ambayo katika matokeo ya mtihani wa kuhitimu darasa la saba uliofanyika
mwaka jana, imefaulisha kwa zaidi ya asilimia 90.
Msaada
huo ni mwendelezo wa shirika hilo kuishika mkono halmashauri ya Wilaya ya
Kasulu ambapo katika siku za karibuni shirika hilo, limeikabidhi
halmashauri ya Wilaya ya Kasulu matundu sita ya vyoo vilivyojengwa kwenye shule
ya msingi ya Kumtundu.
Post a Comment