Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Johari Samizi, ameipongeza taasisi ya kusaidia sekta binafsi ya Kilimo (PASS TRUST) kwa namna inavyochochea maendeleo ya kilimo kwa dhamana ya mikopo inayoitoa kwa wakulima, kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.
Samizi
ametoa pongezi hizo leo tarehe 20.04.2023, wakati akizungumza kwa niaba ya mkuu
wa mkoa wa Shinyanga, katika ufunguzi wa warsha ya siku moja ya kuzindua
Progromu ya KIJANISHA MAISHA katika mkoa wa Shinyanga, iliyokuwa imeandaliwa na
PASS TRUST, iliyowashirikisha wadau mbalimbali wa sekta za kilimo, uvuvi,
ufugaji na mazao ya misitu kutoka wilaya zote za mkoa wa Shinyanga.
Amepongeza
ubunifu uliofanywa na taasisi hiyo kwa kuja na mbinu zinazowawezesha wakulima
kuwekeza kwenye kilimo kinachoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,
badala ya kubaki wakitegemea mvua za msimu, ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuwataka
wakulima wote kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia uhifadhi wa
mazingira, ikiwemo kutokata miti ovyo na kuharibu vyanzo vya maji.
Samizi
amebainisha kuwa, dhamana ya mikopo inayotolewa na taasisi hiyo kwa ajili ya
wakulima na sekta nyingine zinazonufaika na mpango huo, inasaidia kwa kiasi
kikubwa kuwezesha juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuwainua wakulima
wadogo, ili watoke kwenye kilimo cha kujikimu na badala yake waingie katika kilimo
cha kibiashara (kilimobiashara)
Mkuu huyo wa
Wilaya amezitaka taasisi za kifedha zilizoingia ubia na PASS TRUST kutotumia fursa hiyo kuwaumiza
wakulima, kwa kuwatoza kiwango kikubwa cha riba.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara wa PASS TRUST Bw. Adam Kamanda,
amesema taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, imetoa dhamana ya
mikopo yenye thamani ya Shilingi Trioni 1.3 kwa uwekezaji katika sekta za
kilimo, uvuvi, ufugaji na mazo ya misitu, ambapo kwa kanda ya ziwa kwa mwaka
uliopita wa 2022, imedhamini jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 93.1,
huku mkoa wa Shinyanga ukiwa umepata dhamana ya jumla ya Shilingi Bilioni 35.5.
Taasisi ya
PASS TRUST, ilianzishwa mwaka 2000 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Denimark kupitia mpango wa kuwezesha
kilimo ili kusaidia uzalishaji wenye tija, ambapo chini ya mpango uliozinduliwa
hivi karibuni wa KIJANISHA MAISHA, taasisi hiyo imejikita zaidi kudhamini
miradi ambayo imelenga kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo, ili iendane na
sera ya uhifadhi wa mazingira.
Taasisi hiyo
imeingia ubia wa kutoa dhamana ya mikopo kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na
waliowekeza kwenye mazao yatokanayo na misitu na taasisi 14 za kifedha, ikiwemo
Benki za MKOMBOZI, NMB, NBC, CRDB na Vision Fund.

Post a Comment