Wajumbe wa Kamati ya maendeleo ya Kata ya Ndembezi (WDC) katika halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wameuomba uongozi wa Manispaa kupitia wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) kuzifanyia matengenezo barabara za mitaa ambazo hazipitiki, pamoja na kukamilisha mapema zile zilizopo kwenye hatua ya ukarabati.
Wakizungumza kwenye kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kipindi cha robo ya Januari hadi Machi 2023, wamesema barabara nyingi katika mitaa ya Butengwa, Ndembezi, Dome na Tambukareli hazipitiki hasa katika kipindi hiki cha mvua, huku zinazoendelea kukarabatiwa zikiachwa na vifusi kwa muda mrefu na kusababisha usumbufu.
Wameiomba Serikali kupitia TARURA kuzifanyia matengenezo barabara zote za mitaa iliyotajwa, pamoja na kukamilisha kwa wakati zile zilizopo kwenye ukarabati ili kuepuka usumbufu kwa wananchi.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ndembezi Victor Thobias, amesema ataendelea kuwasilisha kilio hicho cha wananchi kwa mamlaka zinazohusika, kupitia vikao vya baraza la madiwani.
Amesema kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa, wataendelea kuzibainisha na kuziwasilisha Serikalini changamoto hizo na nyingine zilizopo ili kuhakikisha zinatatuliwa.
“Tunaendelea kupambana katika kuhakikisha tunailetea maendeleo Kata ya Ndembezi, changamoto zipo ambazo ninazipitia mpaka sasa, waheshimiwa wenyeviti pia tunashirikiana nao changamoto wanazileta na sisi tunazichukua na kuzipeleka Manispaaa na baada ya hapo Manispaa wanaangalia bajeti yao, lakini nashukuru uongozi wa Manispaa wamekuwa wakitusikiliza, kila tukiomba tunapewa japo unaweza kuomba asilimia100% unapewa 75% si haba” amesema Mh. Victor.
Kufuatia hoja hiyo, Mwakilishi wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Shinyanga Mhandisi Julius Maduhu, amesema watafanyia kazi changamoto zilizobainishwa, ikiwemo mapungufu yaliyojitokeza kwa Mkandarasi anayeendelea na shughuli za uboreshaji wa barabara za mitaa.
Awali akiwasilisha taarifa hiyo, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ndembezi Jackson Njau, amesema utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo umefanikiwa kwa kiwango kikubwa, kwa kuwa shule nyingi zimeandikisha watoto zaidi ya kiwango kilichotarajiwa.
Aidha ameitaja miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa kwa kipindi hicho, kuwa ni ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika shule ya Msingi Ndembezi, pamoja na ujenzi wa vyoo viwili vya kisasa katika shule ya Sekondari Mazinge, utakaogharimu kiasi cha Shilingi milioni 58, kwa ufadhili wa mwanamitindo Flaviana Matata.
Post a Comment